SAKATA la mshambuliaji raia wa Ghana, Jonathan Sowah, limeendelea kushika kasi ndani ya Simba SC baada ya mchezaji huyo kuonekana akifanya mazoezi na kikosi cha vijana (U20), hatua iliyotafsiriwa kama sehemu ya adhabu ya kinidhamu.
Uongozi wa Simba uliamua kumshusha Sowah kwenye timu ya vijana ili kumjengea nidhamu na kumuweka sawa kabla ya kurejea kikosi cha kwanza, ukiamini kuwa hiyo ni njia sahihi ya kumsaidia kurekebisha mwenendo wake.
Hata hivyo, hali haikuenda kama ilivyotarajiwa baada ya mshambuliaji huyo kugoma kuendelea na mazoezi hayo kuanzia siku ya pili, jambo lililoibua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki na wadau wa soka.
Taarifa kutoka kwa watu wake wa karibu zinaeleza kuwa Sowah hakuwa tayari kujiunga na timu ya vijana, akiamini kuwa hastahili adhabu hiyo kwa kuwa hana kosa la msingi alilofanya.
Kutokana na msimamo huo, inaelezwa kuwa klabu imeanza kutafuta mbinu mbadala ya kushughulikia suala hilo, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kumalizana naye kwa njia ya kisheria ili kuepuka migogoro inayoweza kufika katika mamlaka za soka za kimataifa.
Kwa upande wake, Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally, amesisitiza kuwa mchezaji huyo anapaswa kuheshimu maamuzi ya klabu na kukubali adhabu hiyo kama sehemu ya kujirekebisha kabla ya kurejea kikosini.
Licha ya sintofahamu hiyo, Sowah bado ana mkataba wa miaka miwili na Simba SC, na msimu huu tayari ameonyesha uwezo wake kwa kufunga mabao matatu katika mechi nne alizocheza, akibaki kuwa mchezaji mwenye mchango muhimu ndani ya timu hiyo.