Home Habari za michezo KAZI IPO, MAEMA ASEMA SIMBA TAYARI KWA MAPAMBANO MAKALI

KAZI IPO, MAEMA ASEMA SIMBA TAYARI KWA MAPAMBANO MAKALI

0

KIUNGO mshambuliaji wa Simba SC, Neo Maema, ameweka wazi dhamira ya timu yake kuelekea mchezo wa fainali ya Kombe la Muungano, akisisitiza kuwa wanatambua ukubwa wa pambano lililopo mbele yao.

Maema amesema kuwa wanaiheshimu Yanga kama mpinzani wao mkubwa, lakini hilo halijawapunguzia ari ya kupambana kuhakikisha wanabeba taji hilo muhimu.

Ameeleza kuwa maandalizi ya kikosi hicho yamekuwa mazuri, huku kila mchezaji akiwa na hamasa ya hali ya juu kuhakikisha wanatoa kiwango bora siku ya mchezo.

“Tunafahamu Yanga ni mpinzani mgumu, lakini tunataka kushinda Kombe la Muungano. Mechi haitakuwa rahisi, kazi kwetu ni kupambana kutafuta matokeo katika fainali,” amesema Maema.

Nyota huyo ameongeza kuwa katika mechi kama hizo za fainali, kinachohitajika zaidi ni umakini, nidhamu na kutumia vizuri nafasi zitakazopatikana ili kufikia malengo yao.

Simba SC inatarajia kuingia uwanjani ikiwa na presha ya kutaka ushindi, huku mashabiki wao wakisubiri kwa hamu kuona timu yao ikifanya vizuri na kuibuka mabingwa.