UONGOZI wa Junguni United inayoshiriki Ligi Kuu Zanziabar, umesema hauna uhakika wa kusafiri kwa ajili ya mechi mbili za mzunguko wa 25 na 26 kutokana na hali mbaya ya kiuchumi waliyonayo.
Hadi sasa katika ligi hiyo zimesalia mechi saba kumaliza msimu na timu hiyo imekuwa ikipitia kipindi kigumu cha kiuchumi na inatakiwaa kusafiri hadi Unguja kwa ajili ya mechi hizo.
Mwandishi wa Soka la Bongo alishuhudia hali ngumu iliyonayo timu hiyo kwa sasa, huku baadhi ya wachezaji waliotoka Tanzania Bara wakilazimika kurudi nyumbani.
Chanzo kutoka ndani cha timu hiyo, kililiambia Mwanaspoti, viongozi hawana uwezo wa kuisafirisha timu kucheza mechi nje ya Pemba, labda wajitokeze wafadhili wa kusaidia nauli.
“Nikwambie tu ukweli, hatuna uhakika wa timu kuisafirisha maana hakuna fedha, hadi sasa viongozi waliokuwa wakishughulikia wachezaji wamekimbia, ukiwapigia simu hawapokei wakati mwingine hawapatikani,” kilisema chanzo hicho na kuongeza; viongozi waliokuwa ndio msaada kwa timu hiyo, wamekaa pembeni baada ya baadhi yao kutumia fedha kinyume na matumizi ya timu.
Kutokana na hali hiyo, mtoa taarifa huyo amesema sio tu timu kushuka daraja, bali wanaiona Junguni United ikipotea mazima kwenye soka la Zanzibar.
Pia, chanzo hicho kilisema mazingira magumu iliyonayo timu, imewalazimu baadhi ya wachezaji kuomba msaada msikitini wapate nauli ya kurudi kwao.
Baada ya timu kuyumba, taarifa zinabainisha, kati ya wachezaji 10 waliosajiliwa, wanane wameondoka na kubaki wawili ambao wamekwama kwa sababu hawajapata nauli za kurudi kwao.
“Hao wachezaji wawili waliobaki wanaingia mitaani kuomba chakula kwa wananchi kwa sababu hawajui pa kuishika maana viongozi wamewatelekeza, hawajui cha kufanya,” kilisema chanzo hicho.
Alipotafutwa Msemaji wa Junguni, Suleiman Sultan Hemed kuzungumzia hali hiyo, amesema: “Timu imeshindwa kujiendesha kutokana na ukosefu wa fedha jambo ambalo limesababisha kuomba misaada kwa wengine bila mafanikio.
“Fedha ndiyo chanzo kikuu cha migogoro ndani ya timu kwani kila mmoja ana mtazamo wake hususani fedha zinazoingizwa na mdhamini wa ligi.”
Junguni imecheza mechi 23 za Ligi Kuu Zanzibar msimu huu, imeruhusu mabao 64 na kufunga 17, ikivuna pointi 10 huku ikiwa nafasi ya 15 kwenye msimamo.