Home Habari za michezo MABULA KUTIMKIA UTURUKI

MABULA KUTIMKIA UTURUKI

0

KUNA uwezekano kiungo wa Kitanzania, Alphonce Mabula anayekipiga Shamakhi FC ya Ligi Kuu Azerbaijan akatimkia Kasımpaşa Spor Kulubu ya Uturuki.

Mabula ambaye alijiunga na Shamakhi dirisha dogo la msimu uliopita akitokea FK Spartak Subotica ya Ligi Kuu ya Serbia alikocheza kwa misimu miwili.

Sasa inaelezwa Kasimpasa inafuatilia kwa ukaribu uwezekano wa kumsajili kiungo huyo wa chini kuelekea msimu ujao.Ikumbukwe Juni mwaka jana Mabula ameongeza mkataba wa mwaka mmoja unaotamatika Juni 30 mwaka huu, hivyo amebakiza miezi miwili tu.Taarifa zinaeleza kuwa mabosi wa klabu hiyo ya Uturuki wamevutiwa na kiwango anachoendelea kukionesha Mabula akiwa na Shamakhi FC, ambapo amekuwa nguzo muhimu katika eneo la kiungo kwa nidhamu, uwezo wa kukaba na kuanzisha mashambulizi.Soka la Bongo ilipomtafuta mtu wa karibu na mchezaji huyo (jina tunalo) amesema tayari timu hiyo imefanya mazungumzo ya awali na menejimenti ya mchezaji ingawa bado hawajafikia makubaliano rasmi.“Ni kweli kuna klabu kadhaa zinafuatilia mwenendo wake, na Kasimpaşa ni moja ya hizo. Wameonyesha kuvutiwa na maendeleo yake hasa msimu huu. Lakini bado hakuna makubaliano rasmi,” amesema mtu huyo wa karibu ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa mchezaji huyo anaangalia kwa umakini mustakabali wake, hasa ikizingatiwa kuwa mkataba wake na Shamakhi unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

“Mkataba wake unaelekea mwisho, hivyo anayo nafasi ya kuchagua kubaki au kwenda sehemu nyingine. Kipaumbele chake ni kupata timu itakayompa nafasi ya kucheza katika kiwango cha juu zaidi na kuendelea kukuza kipaji chake,” ameongeza.

Mabula, ambaye amewahi kuitumikia timu ya taifa ya Tanzania, ameonyesha kiwango kizuri katika ligi ya Azerbaijan, hali iliyomfanya kuanza kuvutia macho ya klabu mbalimbali.

Iwapo dili hilo litafanikiwa, Mabula ataungana na wachezaji wengine wa Kitanzania wanaokiwasha Uturuki akiwemo Novatus Miroshi anayeitumikia Goztepe, Diana Msewa anayekipiga Trabzonspor ya Ligi Kuu Wanawake.