Home Habari za michezo WAMETUPIA SANA MSIMU MMOJA LIGI YA MABINGWA

WAMETUPIA SANA MSIMU MMOJA LIGI YA MABINGWA

0

IKIWA ndio mashindano bora zaidi ya soka kwa ngazi ya klabu duniani kwa sasa, Ligi ya Mabingwa Ulaya imekuwa na namba za aina mbalimbali zilizowekwa na mastaa wa kandanda, lakini ni wachezaji gani waliofunga mabao mengi zaidi katika msimu mmoja wa mashindano hayo?

Hawa ni mastaa wanaotembea na namba bora za kutupia nyavuni kwa msimu mmoja wa mashindano hayo katika misimu tofauti, wakiwa wamefunga mabao mengi zaidi katika shindano moja:

Cristiano Ronaldo 2013-14 (17)

Msimu bora zaidi wa kufunga mabao katika historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ulikuwa 2013-14, ambapo Cristiano Ronaldo wa Real Madrid alifunga mabao 17, akichangia kwa kiasi kikubwa ushindi wa timu yake na kutwaa taji. Ronaldo alianza msimu kwa kasi, akifunga hat-trick katika ushindi wa 6-1 dhidi ya Galatasaray ugenini katika mechi ya kwanza ya makundi, kabla ya kuongeza mabao sita zaidi katika hatua hiyo. Aliendelea kufunga katika hatua ya 16 bora (mabao manne), robo fainali (moja) na nusu fainali (mawili), kabla ya kuhitimisha kwa penalti dakika ya 120 katika ushindi wa 4-1 dhidi ya Atlético Madrid kwenye fainali.

Cristiano Ronaldo 2015-16 (16)

Miaka miwili baadaye, Ronaldo alikaribia kuvunja rekodi yake mwenyewe alipofunga mabao 16 katika msimu wa 2015-16, akiwa njiani kuisaidia tena Real Madrid kutwaa ubingwa. Alifunga mabao 11 katika hatua ya makundi, rekodi ya mchezaji mmoja katika msimu wa Ligi ya Mabingwa. Idadi hiyo ilikuwa mabao mawili zaidi ya mfungaji wa pili bora msimu huo, Robert Lewandowski (mabao tisa). Alianza msimu kwa hat-trick dhidi ya Shakhtar Donetsk, na akamaliza hatua ya makundi kwa kufunga mabao manne dhidi ya Malmo FF. Hakufunga kwenye fainali dhidi ya Atlético Madrid, lakini alifunga penalti ya ushindi katika mikwaju ya penalti, Real Madrid ikitwaa taji mjini Milan.

Ronaldo, Lewandowski, Benzema, Mbappe (15)

Msimu wa tatu bora wa Cristiano Ronaldo ulikuwa 2017-18 alipofunga mabao 15, huku Real Madrid ikishinda taji kwa kuifunga Liverpool 3-1 katika fainali. Nyota huyo hakufunga kwenye fainali, lakini alifunga katika mechi 10 msimu huo akilingana na rekodi yake ya kufunga katika mechi nyingi zaidi za Ligi ya Mabingwa kwa msimu mmoja. Vilevile katika mastaa wenye rekodi ya kufunga mabao 15, Robert Lewandowski aliingia fainali ya 2019-20 akihitaji bao moja kufikia rekodi ya kufunga katika mechi 10 tofauti, lakini hakufanikiwa.

Hata hivyo, Bayern Munich ilishinda bao 1-0 dhidi ya PSG, na Lewandowski alikuwa amefunga mabao 15 katika mechi tisa kabla ya fainali. Katika msimu wa 2021-22, mabao 10 kati ya 15 ya Karim Benzema yalitoka hatua ya mtoano, rekodi iliyokuwa mikonon mwa Ronaldo (2016-17). Alifunga hat-trick dhidi ya PSG, nyingine dhidi ya Chelsea, pamoja na mabao muhimu dhidi ya Manchester City. Hakufunga fainali dhidi ya Liverpool, lakini Real Madrid ilitwaa ubingwa.

Pia kuna Kylian Mbappe ambaye anaingia kwenye orodha hii 2025-26 akiwa mchezaji wa tatu wa Real Madrid kufunga mabao 15 katika msimu mmoja wa Ligi ya Mabingwa. Nyota huyo alianza kwa kasi kubwa akifunga mabao matano katika mechi mbili za kwanza, ikiwemo hat-trick dhidi ya Kairat. Pia alifunga mabao manne dhidi ya Olympiakos na kumaliza hatua ya awali akiwa na mabao 11. Aliendelea kufunga dhidi ya Benfica na Bayern Munich, ingawa Real Madrid ilitolewa katika hatua ya robo fainali.

MABAO MENGI ZAIDI MSIMU MMOJA LIGI YA MABINGWA

Cristiano Ronaldo  (Real Madrid, 2013-14) – 17

Cristiano Ronaldo  (Real Madrid, 2015-16) – 16

Robert Lewandowski        (Bayern Munich, 2019-20) -15

Cristiano Ronaldo  (Real Madrid, 2017-18) – 15

Karim Benzema     (Real Madrid, 2021-22) – 15

Kylian Mbappe        (Real Madrid, 2025-26) – 15

Lionel Messi (Barcelona, 2011-12) – 14

Robert Lewandowski        (Bayern Munich, 2021-22) – 13

Serhou Guirassy    (B. Dortmund, 2024-25)- 13

Raphinha               (Barcelona, 2024-25) – 13

Cristiano Ronaldo  (Real Madrid, 2012-13) – 12

Erling Haaland       (Manchester City, 2022-23) – 12

Lionel Messi (Barcelona, 2018-19) – 12

Cristiano Ronaldo  (Real Madrid, 2016-17) – 12

Ruud van Nistelrooy        (Manchester United, 2002-03) -12

Mario Gomez         (Bayern Munich, 2011-12) – 12

Lionel Messi (Barcelona, 2010-11) – 12