BAADA ya Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Shedrack Nsajigwa kuiongoza timu hiyo katika mechi sita sawa na dakika 540 bila kuonja ushindi, kesho Ijumaa atakuwa na kibarua kizito kuisimamisha TRA United kusaka pointi tatu za kwanza.
Nsajigwa aliyetua kikosini humo kuchukua nafasi ya Zedekiah Otieno raia wa Kenya, katika mechi sita alizosimamia ikiwamo ya Kombe la Shirikisho la CRDB, amepoteza nne na sare mbili, huku kikosi hicho kikikamata nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa pointi 14.
Mechi alizopoteza ni dhidi ya Yanga waliokutana mara mbili akifa 3-0 na 1-0, Singida Black Stars 2-1 na Mbuni FC ya Championship iliyoshinda 1-0 katika mchezo wa Kombe la CRDB hatua ya 16 bora, huku ikitoa sare mbele ya KMC 1-1 na Azam FC.
TRA United iliyopo nafasi ya sita kwa pointi 27, haijapoteza mechi katika michezo minne mfululizo ikiwa ni ushindi tatu ikiwamo Kombe la Shirikisho la CRDB na sare moja, kesho itakuwa ikijiuliza dhidi ya Maafande hao wa Magereza, mchezo ukipigwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Rekodi kwa timu hizo zinaonyesha zimekutana mara tano ambapo TRA United (zamani Tabora United) imeshinda michezo miwili, ikipoteza mmoja na sare mbili na sasa hesabu za wapinzani hao ni kusaka pointi tatu kujiweka nafasi nzuri.
Pia kwa sasa TRA United chini ya Kocha raia wa Burundi, Ettiene Ndayiragije imeonekana kuwa bora, huku nyota wake machachari Ramadhan Salum ‘Chobwedo’ akiiteka Ligi Kuu kwa vitu vyake uwanjani.
Akielezea maandalizi ya mchezo huo, Nsajigwa amesema anafahamu ugumu lakini umuhimu wake katika kuinasua timu nafasi za chini akisema nyota wa kikosi hicho wameonesha matumaini ya kushinda baada ya kusota muda mrefu.
Amesema maboresho aliyofanya kikosini anaamini vijana watatumia vyema nafasi kupata mabao ambayo kimsingi ndio kiu yao kuhakikisha wanarejesha matumaini kikosini na hata kwa mashabiki nje ya uwanja.
“Tumekuwa na muda mzuri wa maandalizi na tunajua ugumu wa wapinzani, vijana wako tayari kwa ajili ya mechi hiyo na niombe mashabki waje kwa wingi kutusapoti,” amesema Nsajigwa.