Home Habari za michezo MAKONDA ASISITIZA UMAKINI WA WAAMUZI LIGI KUU BARA

MAKONDA ASISITIZA UMAKINI WA WAAMUZI LIGI KUU BARA

0

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, ameitaka Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) na wadau wa soka nchini kuongeza umakini katika usimamizi wa waamuzi, akisisitiza kuwa nidhamu ni msingi muhimu wa kuhakikisha michezo inachezwa kwa haki na ufanisi.

Makonda ameyasema hayo leo Aprili 30, 2026 katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yaliyofanyika jijini Arusha.

Kauli ya Makonda inajiri baada ya mwamuzi kutoka Kenya, Dickens Mimisa Nyagrowa aliyechezesha Dabi ya Kariakoo ambayo Simba iliichapa Yanga bao 1-0, Aprili 29, 2026 kwenye fainali ya Kombe la Muungano, kusifiwa kwa kufanya vizuri, jambo ambalo amesisitiza siyo afya kwa soka la Tanzania.

Makonda amesema ameridhishwa na kiwango cha mchezo huo, huku akibainisha maeneo ya kuboreshwa hususani kwa waamuzi akiona kuna changamoto kubwa.

“Nawapongeza sana Watanzania wote waliongalia mpira, sina maana ya walioshinda pekee, bali wote. Kwa kweli ulikuwa mpira mzuri sana,” amesema.

Ameitaka Bodi ya Ligi Tanzania kuongeza umakini katika upangaji na usimamizi wa waamuzi, akisisitiza umuhimu wa maadili na nidhamu katika kuhakikisha haki inatendeka uwanjani.

“Tunataka umakini wa hali ya juu kwa waamuzi wetu. Haipendezi kuona Watanzania wanampongeza refa wa nje wakati tuna waamuzi wetu. Hii inaonyesha kuna tatizo linalohitaji kufanyiwa kazi,” amesisitiza.

Makonda ameongeza kuwa malalamiko dhidi ya waamuzi yamekuwepo kwa muda mrefu, hivyo ni muhimu hatua zichukuliwe ili kulinda hadhi ya soka la Tanzania.

Ameeleza kuwa, hata utoaji wa kadi katika mchezo huo ulikuwa na utofauti, jambo lililowavutia mashabiki kutokana na utaratibu uliotumika.

Waziri huyo ametangaza kuwa mfumo wa teknolojia ya msaada wa maamuzi ya video (VAR) utaanza kufungwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha na Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Dar es Salaam ili kusaidia waamuzi kufanya maamuzi sahihi.

“Tunawahakikishia kuwa VAR inakuja. Mwamuzi akijichanganya, atapata nafasi ya kupitia upya tukio kwa msaada wa teknolojia,” amesema Makonda.