Yanga inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 47 ikiiacha Simba nafasi ya pili na pointi 42, huku timu zote zikicheza mechi 19.
Dabi hiyo ya Jumapili kila upande inaitazama kwa jicho la karibu zaidi kwani ushindi utabadili hali ilivyo kwenye msimamo.
Wakati hali ikiwa hivyo Yanga, mabosi wa Simba wao wamefanya uamuzi wa haraka kuiwahisha timu Dar es Salaam ili kufanya maandalizi ya mechi ya Jumapili ambayo watakuwa wenyeji.
Katika uamuzi huo, mara tu baada ya mechi ya fainali ya Kombe la Muungano kumalizika sambamba na sherehe zote za kukabidhiwa kombe kufanyika, baadhi ya wachezaji na viongozi wa benchi la ufundi la timu hiyo walirejea Dar fasta kwa usafiri wa ndege, huku wengine wakirejea na boti.
Taarifa ambazo Mwanaspoti ilizipata kutoka Simba, wameamua kufanya hivyo ili kupata muda mzuri zaidi wa kujiandaa kwani bado wana uhitaji wa kushinda mechi hiyo nyingine.
“Wachezaji ambao walianza katika mechi dhidi ya Yanga, waliondoka mapema kwa ndege kurejea Dar es Salaam wakiwa na baadhi ya viongozi wa benchi la ufundi, kisha wale ambao hawakupata muda mwingi wa kucheza au ambao hawakucheza kabisa, walirejea na boti wakiwa na kombe.
“Tumefanya hivyo ili kuwawahisha wachezaji kuja kupumzika, kisha kuanza mara moja maandalizi ya mechi ya Jumapili ambayo pia bado tunahitaji ushindi,” amesema kiongozi mmoja wa Simba.