KOCHA Mkuu wa Simba, Steven Barker, amesema bado wana nafasi kubwa ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara licha ya tofauti ya pointi tano dhidi ya watani wao Yanga.
Barker ameweka wazi kuwa ndani ya kipindi cha wiki moja, hali ya msimamo inaweza kubadilika na pengo hilo kufutika, akisisitiza kuwa ligi bado iko wazi kutokana na wingi wa mechi zilizosalia.
Kauli ya kocha huyo inaashiria matumaini ya Simba kuzidi kupambana huku wakihitaji matokeo chanya, pamoja na wapinzani wao kupoteza pointi ili kurahisisha safari ya kufikia kileleni.
Hata hivyo, ameweka msisitizo kuwa timu yake inapaswa kwanza kufanya kazi yake uwanjani.
Licha ya sare katika mchezo wa Kariakoo Derby uliowakosesha alama mbili muhimu, Barker anaamini matokeo hayo hayajafuta ndoto zao za ubingwa.
“Bado tupo kwenye kinyang’anyiro, kuna mechi nyingi mbele. Hii ligi unaweza kuona tofauti ya pointi tano ikifutika hata ndani ya wiki moja,” amesema Barker.
Ameongeza kuwa mzunguko wa pili bado una mechi nyingi, jambo linalotoa nafasi kwa timu yake kurekebisha makosa na kukusanya pointi muhimu katika mbio za ubingwa.