Home Habari za michezo STRAIKA POLISI TANZANIA AFICHUA JAMBO CHAMPIONSHIP

STRAIKA POLISI TANZANIA AFICHUA JAMBO CHAMPIONSHIP

0

NYOTA wa maafande wa Polisi Tanzania, Naku Kazimoto amesema licha ya kutoifikia rekodi yake ya mabao ya msimu wa 2024-2025, ataendelea kupambana ili kutimiza malengo waliyojiwekea ya kuirejesha timu hiyo Ligi Kuu Bara.

Akizungumza na Soka la Bongo, Naku amesema licha ya kubaki mechi sita za kumaliza msimu, ni ngumu kwake kufikia rekodi ya msimu uliopita kutokana na ushindani mkubwa wa nafasi katika eneo la ushambuliaji la kikosi hicho.

“Ni ngumu sana kutimiza malengo yangu ya kufikisha zaidi ya mabao 10 kwa sababu ya kukosa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza mara kwa mara, kwa sasa nitapambana kwa ajili ya timu ili ipande Ligi Kuu msimu ujao,” amesema Naku.

Aidha, amesema ushindani uliopo msimu huu ndiyo siri kubwa ya timu hiyo pia kupambana kutimiza malengo ya kuirudisha Ligi Kuu, licha ya mwanzoni mwa msimu kuanza vibaya kutokana na uwepo wa wachezaji wengi wapya.

“Tulianza vibaya sana mwanzoni mwa msimu lakini ilichangiwa na wachezaji wengi walikuwa wapya na aina ya uchezaji wetu bado ulikuwa changamoto, tunashukuru tumekaa kwa muda mrefu na matunda yake tunaanza kuyaona kadri tunavyozidi kucheza.

Nyota huyo mwenye mabao matatu msimu huu, kabla ya kujiunga na Polisi Tanzania alicheza Mbuni FC ya jijini Arusha, ambayo msimu wa 2024-2025, alimaliza kinara katika kikosi hicho baada ya kufunga mabao 12.

Mshambuliaji huyo alijiunga na Mbuni FC dirisha dogo la Januari 2024, baada ya kuonyesha kiwango kizuri akiwa na Copco FC cha jijini, Mwanza na msimu wa 2023-2024, aliifungia timu hiyo ya Arusha mabao 10.