Home Habari za michezo STRAIKA DODOMA JIJI ASAKA REKODI MPYA

STRAIKA DODOMA JIJI ASAKA REKODI MPYA

0

MSHAMBULIAJI wa Dodoma Jiji, Edgar William amefikisha mabao sita ya Ligi Kuu Bara msimu huu akiwa na kikosi hicho sawa na aliyofunga msimu wa 2024-2025, akicheza Fountain Gate, huku akihitaji bao moja kuandika rekodi mpya.

Bao hilo la sita kwa nyota huyo amelifikisha Mei 6, 2026 baada ya kuifunga Mtibwa Sugar katika ushindi ilioupata Dodoma Jiji wa 1-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Akizungumza na Soka la Bongo, Edgar aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Fountain Gate, amesema amepata morali mpya kwa kufunga bao hilo la ushindi kwa kikosi hicho, hasa baada ya kuandamwa na ukame wa muda mrefu.

“Nadhani ilikuwa ni suala la muda kwangu kuanza kufunga tena baada ya kukaa muda mrefu, ni jambo la kawaida kwa mtu yeyote hasa mshambuliaji, ila nashukuru niko katika mstari mzuri wa kuvunja rekodi yangu pia niliyoweka,” amesema Edgar.

Kabla ya kutua Dodoma Jiji, msimu wa 2024-2025 Edgar aliifungia Fountain mabao sita katika Ligi Kuu na kuasisti mawili, huku akikumbukwa msimu wa 2023-2024, alipokuwa mfungaji bora wa Championship akiwa na KenGold baada ya kufunga mabao 21.

Mbali na ufungaji bora, Edgar alishinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Championship msimu wa 2023-2024, akiwashinda Casto Mhagama aliyecheza naye KenGold na Mganda Boban Zirintusa, aliyekuwa Biashara United.

Nyota huyo anashikilia rekodi nzuri katika Ligi ya Championship kwani licha ya kuibuka mchezaji bora na mfungaji bora, pia amepandisha timu mbili Ligi Kuu Bara, akianza na Mbeya Kwanza msimu wa 2021-2022, kisha KenGold msimu wa 2023-2024.