KOCHA Mkuu wa Hausung FC ya Njombe, Selemani Kitunda Simota ‘Guardiola’, amesema licha ya timu hiyo kutokuwa na mechi yoyote hadi Aprili 17, wachezaji wa kikosi hicho hawatakuwa na muda wa kupumzika na wataendelea na mazoezi.
Akizungumza na Soka La Bongo, Guardiola amesema katika mechi sita zilizobaki hawana muda wa kutoa mapumziko kwa wachezaji kutokana na nafasi mbaya waliyopo, hivyo wataendelea na mazoezi ili kufanyia kazi changamoto mbalimbali zilizopo.
“Malengo yetu kwa sasa ni kuinusuru timu na janga la kushuka daraja na mwenendo wetu siyo mzuri, tuna mechi sita kabla ya kumaliza msimu sawa na pointi 18, ambazo naamini tukizipata tutakuwa tumetoka nafasi hizi za chini,” amesema Kitunda.
Kitunda anayefananishwa na Kocha wa Manchester City ya England, Pep Guardiola, katika karia yake ya soka amecheza timu mbalimbali za Kikwajuni FC, Polisi Pemba na Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo maarufu KMKM FC zote za visiwani, Zanzibar.
Kitunda amewahi pia kuzifundisha Tunduru Korosho, Stand United ‘Chama la Wana’, Cosmopolitan na mabingwa wa Ligi Kuu mwaka 1982, Pan Africans.
Hausung imepanda daraja msimu huu na kushiriki Championship baada ya kuongoza kundi A na pointi 25, ikiungana na mabingwa wa Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2024-2025, Gunners FC ya Dodoma, iliyoongoza pia kutoka kundi B na pointi 35.
Timu hiyo inayotumia Uwanja wa Amani uliopo Mkoa wa Njombe, katika mechi 23, ilizocheza msimu huu imeshinda tatu, sare mbili na kupoteza 18, ikishika nafasi ya 15 na pointi 11, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 15 na kuruhusu 45.