Habari za michezo
CHAMA AIPONZA YANGA, MENEJA AFUNGIWA MECHI TATU
Vardo
May 11, 2026
11:56 am
BAADA ya matukio yaliyotokea kwenye dabi ya Kariakoo kati ya Yanga SC na Simba SC, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeichukulia hatua kali Yanga kwa kuipa adhabu mbalimbali zenye uzito mkubwa.
Maamuzi hayo yalifikiwa katika kikao cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi kilichofanyika kufuatia matukio yaliyojitokeza katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2 Mei 3 mwaka huu.
Adhabu kubwa zaidi imekuwa ni faini ya Shilingi milioni 30 kutokana na Yanga kuchelewa kuwasili uwanjani kwa dakika tano tofauti na muda uliopangwa. Kwa mujibu wa taarifa ya TPLB, timu hiyo ilitakiwa kufika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo saa 10:30 alasiri lakini ikawasili saa 10:35, jambo lililotajwa kukiuka Kanuni ya 17:15 ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Inaelezwa kuwa sababu ya kuchelewa huko ilitokana na wachezaji pamoja na baadhi ya maofisa wa Yanga kukataa kutumia chumba rasmi cha kuvalia na badala yake kuelekea katika nyumba iliyopo nje ya uwanja upande wa pili wa barabara.
TPLB imesisitiza kuwa licha ya sababu zilizotolewa na klabu hiyo kuhusu usalama, taratibu za mchezo zinapaswa kuheshimiwa bila kuvunjwa.
Mbali na adhabu hiyo ya kifedha, Meneja wa Yanga, Walter Harrison, naye amepewa adhabu kali baada ya kupatikana na kosa la kumsukuma kiungo wa Simba, Clatous Chama, ndani ya eneo la mchezo.
Kamati hiyo imemfungia Harrison kushiriki michezo mitatu pamoja na kumtoza faini ya Shilingi milioni moja kwa kitendo hicho kilichokiuka Kanuni ya 45:2(2.1).
Katika hatua nyingine, shabiki wa Yanga aliyejitambulisha kwa jina la Mohamed Ally Mposo naye amepewa adhabu ya kufungiwa kuingia uwanjani kwa muda wa miezi 12.
TPLB imesema shabiki huyo aliingia katika eneo la kuchezea wakati wa mapumziko na kumwaga viminika, kitendo kilichotafsiriwa kuwa na viashiria vya imani za kishirikina.
Kwa ujumla, adhabu hizo zimeifanya Yanga kubeba mzigo wa gharama za Shilingi milioni 31 huku pia ikipewa pigo la kukosa huduma ya meneja wake kwa michezo mitatu ijayo. Tukio hilo limeibua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki na wadau wa soka kuhusu nidhamu na usimamizi wa mechi kubwa za ligi kuu.
Yanga kwa upande wake ilieleza kuwa kulikuwa na hofu ya kiusalama katika eneo lao la kuvalia, hali iliyochangia maamuzi ya kuchelewa kushuka uwanjani. Hata hivyo, TPLB imeweka wazi kuwa sababu hiyo haiwezi kuhalalisha uvunjifu wa kanuni za mashindano ambazo zinapaswa kufuatwa na kila klabu bila upendeleo.
Dabi ya Kariakoo ya Mei 3 sasa imeendelea kubeba gumzo kubwa hata baada ya dakika 90 kukamilika. Mbali na sare ya mabao 2-2 iliyopatikana uwanjani, mchezo huo umeacha majeraha mengine nje ya uwanja kwa Yanga ambayo sasa italazimika kupambana nayo huku ikiendelea na harakati za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara