RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, ameipongeza Timu ya Soka ya Taifa Tanzania kwa Wanawake chini ya umri wa miaka 20, Tanzanite Queens kwa kufuzu Kombe la Dunia U-20, fainali zitakazofanyika nchini Poland, Septemba 2026.
Dk Mwinyi amesema ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cameroon katika mchezo uliochezwa Mei 10, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, umeonesha kiwango kikubwa cha uzalendo, nidhamu, kujituma na ari ya ushindi kwa vijana kuipeperusha bendera ya Tanzania kimataifa.
“Nawapongeza kwa dhati wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa Timu ya Taifa ya Wasichana chini ya umri wa miaka 20, Tanzanite Queens U-20, kwa kufuzu Kombe la Dunia la Wasichana U-20 litakalofanyika nchini Poland mwezi Septemba mwaka huu,” amesema Dk Mwinyi.
Ameeleza kuwa, mafanikio haya ni hatua kubwa kwa maendeleo ya soka la wanawake nchini na yameleta heshima kubwa kwa taifa letu.
Amesema, timu hiyo imeandika historia na kuwapa matumaini na hamasa vijana wengine hususani wasichana, katika kufikia ndoto zao kupitia michezo.
Pia, Dk Mwinyi amewahimiza kuendelea kufanya maandalizi mazuri, kuongeza nidhamu na kujituma zaidi kuelekea mashindano ya Kombe la Dunia ili kulitangaza taifa kwa mafanikio.
Vilevile, amewapongeza mashabiki na Watanzania kuendelea kuiunga mkono na kuipa hamasa timu hiyo katika safari hii ya kihistoria.
Rais Mwinyi, amesema, kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi wa Zanzibar anawapongeza Tanzanite Queens U-20 kwa mafanikio haya makubwa ya kihistoria.