Habari za michezo

DAKIKA 180 ZA DHAHABU ARSENAL IKIWABEBA WANNE

Vardo May 11, 2026 11:42 am

ARSENAL ina dakika 180 mkononi za dhahabu ambazo zitaamua ukame wa miaka 22 bila taji la Premier League unakoma au itaendelea kusubiri tena kwa msimu mwingine.

Dakika hizo 180 ni sawa na mechi mbili dhidi ya Burnley (nyumbani, Mei 18) na Crystal Palace (ugenini, Mei 24), ambapo Arsenal inahitaji kushinda zote ili kubeba ubingwa bila ya kuangalia matokeo ya mpinzani wake wa karibu, Manchester City yenye mechi tatu mkononi dhidi ya Crystal Palace (nyumbani, Mei 13), Bournemouth (ugenini, Mei 19) na Aston Villa (nyumbani, Mei 24).

Hiyo imekuja baada ya bao la ushindi la kuchelewa la Leandro Trossard likiisogeza Arsenal karibu zaidi na ubingwa wa Premier League huku likiiweka West Ham United kwenye hatari kubwa ya kushuka daraja baada ya mchezo uliokuwa na mwisho wa kusisimua ukichezwa Uwanja wa London.

Arsenal ilikuwa ikihangaika kuipenya safu ya ulinzi ya West Ham hadi dakika za mwisho, ambapo Trossard aliyepiga mpira mara mbili kwenye mwamba wa goli ndani ya sekunde chache kipindi cha kwanza, alikuja kufanikiwa kwa shuti lililomgonga Tomas Soucek na kujaa wavuni dakika ya 83.

Bao hilo lilikuja muda mfupi baada ya kipa wa Arsenal, David Raya, kufanya sevu muhimu dhidi ya Mateus Fernandes, ushindi huo ukiifanya Arsenal kuongoza kwa tofauti ya pointi tano dhidi ya Manchester City ambayo bado ina mchezo mmoja mkononi ili kulingana na wote kubaki na miwili kuhitimisha msimu.

West Ham ilidhani imesawazisha katika dakika za majeruhi, lakini bao la Callum Wilson lilikataliwa baada ya uchunguzi mrefu wa VAR kubaini kulikuwa na madhambi dhidi ya Raya, jambo lililowakasirisha mashabiki wa nyumbani.

Huenda huu ukawa mojawapo ya uamuzi wenye athari kubwa zaidi kuwahi kufanywa na VAR katika historia ya Premier League, kutokana na madhara yake kwenye mbio za ubingwa na vita vya kushuka daraja.

Uamuzi huo uliwapa Arsenal furaha kubwa, lakini kwa West Ham hali ilikuwa tofauti kabisa kwani sasa ipo kwenye nafasi za kushuka daraja, ikiwa pointi moja nyuma ya Tottenham Hotspur pia ikicheza mchezo mmoja zaidi.

Arsenal ilitawala mwanzo wa mchezo, lakini ilipoteza kasi baada ya kocha Mikel Arteta kumhamishia Declan Rice kucheza beki wa kulia kufuatia Ben White kuumia goti.

Rice alirejea katikati kipindi cha pili, lakini West Ham wakaanza kujiamini zaidi, na ilihitaji sevu nyingine muhimu kutoka kwa Raya ambaye pia alikuwa ameokoa kichwa cha Taty Castellanos kumzuia Fernandes aliyekuwa karibu kufunga.

Baadaye Trossard akafunga bao muhimu la ushindi, huku bao la Wilson likikataliwa kutokana na faulo dhidi ya Raya, matokeo yaliyoiweka Arsenal ambayo tayari imefuzu fainali ya UEFA Champions League, pia ikiwa karibu na ubingwa wao wa kwanza Premier League baada ya miaka 22.

Endapo Arsenal itabeba ubingwa wa Premier msimu huu, maana yake ni kwamba itahitimisha ukame huo wa miaka 22 ambapo mara ya mwisho timu hiyo iliposhinda msimu wa 2003–2004 bila ya kupoteza, nyota wanne wa sasa walikuwa hawajazaliwa.

Nyota hao ni kipa Tommy Setford aliyezaliwa Machi 13, 2006 (miaka 20), beki Cristhian Mosquera aliyezaliwa Juni 27, 2004 (miaka 21) ikiwa ni siku 43 tangu ubingwa huo upatikane, beki Myles Lewis-Skelly aliyezaliwa Septemba 26, 2006 (miaka 19) na winga Max Dowman aliyezaliwa Desemba 31, 2009 (miaka 16).

HANS FLICK AIPA UBINGWA BARCA SAA CHACHE BAADA YA KUFIWA RAIS MWINYI AIPONGEZA TANZANIA QUEENS KUFUZU KOMBE LA DUNIA