KIUNGO wa Tanzania, Malaika Meena ameanza kuonyesha kiwango kikubwa katika soka la wanawake Ulaya baada ya kupata muendelezo mzuri tangu ajiunge na Ipswich Town Women kwa mkopo akitokea Bristol City Women.
Nyota huyo mwenye asili ya Tanzania lakini aliyezaliwa England amekuwa mmoja wa wachezaji wanaofuatiliwa kwa karibu kutokana na kiwango chake kinachokua siku baada ya siku.
Kwa sasa Malaika anacheza kwa mkopo Ipswich Town akitokea Bristol City Women inayoshiriki ligi daraja la pili England maarufu ‘Women’s Super League 2’.
Malaika alisajiliwa na Bristol City kwa mkataba wa miaka miwili na nusu baada ya kufanya vizuri akiwa Marekani katika timu ya chuo ya Wake Forest Demon Deacons. Klabu hiyo iliona uwezo wake na kuuendeleza kwa mustakabali wa baadae kwenye soka la wanawake England.
Akiwa Bristol City, kiungo huyo alicheza jumla ya mechi 20 katika mashindano mbalimbali na kufunga bao moja.
Msimu wa 2024/25 alicheza mechi saba na kufunga bao moja kabla ya msimu huu wa 2025/26 kucheza mechi 13 bila kufunga bao.
Takwimu hizo zilitosha kuonyesha uwezo wake wa kucheza eneo la kiungo huku akiongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji.
Baada ya ushindani kuongezeka Bristol City, uongozi wa klabu uliamua kumpeleka kwa mkopo Ipswich Town ili apate nafasi zaidi ya kucheza mara kwa mara.
Hata hivyo, tangu ajiunge na Ipswich, Malaika ameanza kupata dakika nyingi zaidi na kuonyesha muendelezo mzuri wa kiwango chake ndani ya ligi hiyo.
Msimu huu tayari amecheza mechi tano za ligi huku baadhi ya mechi akianza kikosi cha kwanza. Katika mechi dhidi ya Sunderland alicheza dakika zote 90 akiibuka nyota wa mechi, jambo lililoonyesha benchi la ufundi linaanza kumuamini zaidi katika kikosi hicho.
Malaika ambaye alipitia akademi za Arsenal na Chelsea kabla ya kwenda Marekani, anaonekana kuwa sehemu ya kizazi kipya cha wachezaji wanawake wenye asili ya Tanzania wanaofanya vizuri nje ya nchi.
Kiungo huyo aliitwa Timu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars kwa mara ya kwanza kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Tunisia na Botswana hiyo ikiwa nia mara yake ya kwanza kuitwa timu ya taifa.
Kutokana na kiwango kizuri, Malaika aliendelea kuaminiwa na benchi la ufundi la Twiga Stars baada ya kuitwa kwa mara nyingine kwenye kikosi kilichoiondoa Equatorial Guinea kwenye mechi za kufuzu Wafcon 2026.
Hata hivyo, Machi mwaka jana kiungo huyo aliitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa Uingereza chini ya miaka 23.