Habari za Michezo leo
Habari za michezo

MHHHH…HII YA CHAMA NA OKELLO NI SAWA NA PIGA NIKUPIGE….

admin May 15, 2026 6:38 pm

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Allan Okello na Clatous Chama wa Simba, wameanzisha ligi yao kufuatia kila mmoja kufunga katika michezo mitatu mfululizo ya Ligi Kuu Bara, huku Mossi Nduwumwe wa Singida Black Stars naye akiingilia kati bato hiyo.

Licha ya mabao yake mawili juzi Jumatano dhidi ya Dodoma Jiji yakishindwa kuifanya Yanga kuendeleza rekodi yake kwa kucheza mechi 43 bila ya kupoteza, yalimfanya Okello ambaye ni raia wa Uganda kujibu mapigo kwa Chama.

Kabla ya mechi hiyo ambayo ilishuhudiwa Yanga ikikumbana na kipigo cha mabao 3-2, Chama ndiye mchezaji ambaye alikuwa amefunga katika mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga (2-2), JKT Tanzania (1-0) na Tanzania Prisons (4-0) pia alitoa asisti dhidi ya Yanga, akafunga tena dhidi ya JKT Tanzania kisha akafanya tena balaa kwa kufunga na kutoa asisti dhidi ya Prisons, hivyo alihusika katika mabao matano ya Simba kati ya saba.

Hii ni awamu ya pili kwa Chama kuichezea Simba, alirejea Msimbazi akitokea Singida Black Stars akiwa na mabao mawili aliyofunga akiwa na timu hiyo lakini hadi sasa ana mabao sita na asisti nne akiwa ni mmoja kati ya wachezaji muhimu zaidi kwenye kikosi cha timu hiyo msimu huu.

Kama ilivyo kwa Chama, Okello ambaye ni mchezaji bora wa Ligi Kuu Bara mwezi Aprili 2026, amefanya balaa dhidi ya KMC (1-0), Coastal Union (3-0) ya Tanga na Dodoma Jiji ambayo walipoteza kwa mabao 3-2.

Okello ambaye alitua Yanga akitokea Vipers ya Uganda, alifunga dhidi ya KMC, akacheka na nyavu mara mbili dhidi ya Coastal na kutoa asisti moja huku akifunga mara mbili dhidi ya Dodoma Jiji, hivyo amehusika na mabao yote ya Yanga katika mechi hizo.

Huyu ndiye mchezaji mwenye ufanisi zaidi wa kutumia nafasi kwenye kikosi cha Yanga kwa sasa, kiujumla amehusika na mabao 14, akifunga saba na asisti saba ingawa alianza msimu kwa kucheza michezo bila kufunga wala kutoa pasi ya bao.

Kwa upande wa Mossi naye ameingia anga hizo kwa kuuwasha moto katika mechi tatu zilizopita za Singida Black Stars kwa kufunga mabao matano, alifunga moja dhidi ya Namungo, akafunga mara mbili dhidi ya Mtibwa Sugar wakati walima alizeti hao wakiibuka na ushindi wa mabao 4-0.

Mrundi huyo pia alifunga mawili dhidi ya Pamba Jiji wakati Singida Black Stars ikiibuka na ushindi wa mabao 3-1. Hadi sasa amefunga mabao manane na ndiye kinara wa mabao wa Singida Black Stars hadi sasa.

Jambo kuvutia zaidi kwa wachezaji hao ni kwamba wote wametua kipindi cha usajili wa dirisha dogo Januari 2026 na wanaonekana kuwa moto wa kuotea mbali katika kipindi hiki cha lala salama kuelekea mwisho wa msimu huku wakiongeza nguvu kwenye vikosi vyao katika mbio za ubingwa na vita ya nafasi nne za juu.

FEI HAYUPO NYUMA

Licha ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ kutofunga katika michezo mitatu mfululizo iliyopita, kocha wa zamani wa Yanga na Azam, Hans van der Pluijm amemtaja fundi huyo kuwa daraja moja na wachezaji hao.

Fei Toto mwenye mabao 10 na asisti saba kwenye ligi hadi sasa, alifunga katika mechi mbili kati ya tatu zilizopita ambapo mawili dhidi ya Mtibwa Sugar, moja dhidi ya Namungo huku mambo yakiwa magumu dhidi ya TRA United wakati Azam ikichapwa 4-1, bao lao lilifungwa na Jephte Kitambala.

“Nimekuwa nikifuatilia ambacho kinaendelea Tanzania, navutiwa na ushindani uliopo, ndio Okello ni mchezaji mzuri na ameongeza kitu Yanga lakini ni muhimu pia kuona kile ambacho anafanya Fei akiwa na Azam,” amesema na kuongeza; “Kwa Chama ni muendelezo wa ubora na nampongeza kwa kuendelea kuonyesha kuwa yeye ni mchezaji wa daraja gani.”

ZA NDAAANIII KABISAAA…..MASTAA HAWA 6 ‘HAWANA CHAO’ NDANI YA YANGA LIGI IKIISHA…