Habari za michezo
BARKER SIMBA SASA NI FULL MOTO UWANJANI
Vardo
May 17, 2026
1:09 pm
Simba SC imeanza kuonyesha dalili za kurejea kwenye ubora wake wa kawaida chini ya kocha mkuu Steve Barker, baada ya kikosi hicho kuonesha kiwango bora cha soka kinachowapa matumaini makubwa mashabiki wa klabu hiyo.
Katika mechi za hivi karibuni, Simba imekuwa ikicheza kandanda la kuvutia zaidi, likijumuisha kasi ya kushambulia, umiliki mzuri wa mpira pamoja na pasi za uhakika, huku pia ikiongeza presha ya juu uwanjani inayowalazimisha wapinzani kufanya makosa.
Mwenendo huo mpya unaonekana kuwa matokeo ya maboresho ya kiufundi ndani ya timu, ambapo wachezaji sasa wanaelewa kwa kina majukumu yao uwanjani na kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu tofauti na mwanzo wa msimu.
Akizungumzia mabadiliko hayo, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema mashabiki wana kila sababu ya kufurahia maendeleo yanayoonekana ndani ya kikosi hicho, akisisitiza kuwa timu ipo kwenye mwelekeo sahihi wa ushindani.
“Ile Simba ambayo tulikuwa tukiitamani siku zote imerejea. Hii ndio Simba ambayo tulikuwa tukiimba kwa miaka mingi, ile ambayo inaburudisha na kucheza mpira mzuri,” amesema.
Ameongeza kuwa Simba ya sasa imeanza kurudisha heshima yake kwa kucheza soka la kuvutia ambalo hata wapinzani wanapata wakati mgumu kulikabili, jambo linaloongeza hofu kwa timu pinzani.
Kauli hiyo imeongeza hamasa kubwa kwa mashabiki wa Simba, ambao sasa wanaamini kuwa timu yao ipo katika njia sahihi ya kurejea kwenye ushindani wa ubingwa na kuendelea kuwa tishio katika mashindano yote wanayoshiriki