BAO la dakika ya 90 la mshambuliaji wa TRA United, Shaaban Idd Chilunda, limetosha kuipa ushindi timu hiyo wa mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar, katika mechi kali na ya kusisimua ya mzunguko wa 24 wa Ligi Kuu Bara.
Katika mechi hiyo iliyopigwa leo Mei 20, 2026 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Mtibwa Sugar ilitangulia kupata bao la mapema dakika ya pili kupitia Said Mkopi aliyetumia vizuri mpira uliopigwa na kiungo, Fredrick Magata.
Bao hilo liliiamsha TRA na kujibu mapigo ya kutengeneza mashambulizi, ambapo dakika ya tisa ilisawazisha kupitia beki Mganda, Christopher Tebandeke aliyepiga shuti kali akiwa nje ya eneo la 18 na kumshinda kipa, Toba Kutisha.
Wakati mechi hiyo ikionekana inamalizika sare ya 1-1, Chilunda akaibuka shujaa dakika ya 90, baada ya kufunga bao akitumia vizuri pasi ya nyota, Ramadhan Salum ‘Chobwedo’.
Ushindi huo umeifanya TRA United kulipa kisasi, baada ya mechi ya raundi ya kwanza iliyopigwa Novemba 29, 2025, Mtibwa Sugar kushinda kwa mabao 2-1, yaliyofungwa na Kassim Shaibu ‘Mayele’ dakika ya 40 na Ismail Mhesa dakika ya 89.
Katika mechi hiyo, bao la TRA United lilifungwa na Adam Adam dakika ya 11, likiwa ni pambano lililokuwa na ushindani wa hali ya juu kutokana na ubora wa wachezaji wa pande zote mbili.
Ushindi wa leo kwa TRA United umekuja baada ya kucheza mechi mbili mfululizo bila ya kupata pointi tatu, ikianza na sare ya bao 1-1 dhidi ya JKT Tanzania katika Ligi Kuu, kisha kuchapwa na Simba mabao 4-0, kwenye robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB.
Matokeo hayo yanaifanya TRA United kufikisha pointi 37, ikipanda nafasi moja kutoka ya sita hadi ya tano baada ya kushinda mechi 10, sare saba sawa na ilizopoteza, huku Mtibwa ikiwa nafasi ya 10 na pointi 26, ikishinda sita, sare nane na kupoteza 10.