SAO PAOLO, BRAZIL: FAMILIA ya nyota wa Chelsea, Joao Pedro pamoja na marafiki zake wameelezea hasira na masikitiko yao baada ya mshambuliaji huyo kuachwa katika hali ya kushangaza kwenye kikosi cha Brazil kitakachoshirikia Kombe la Dunia 2026.
Licha ya kuwa na msimu bora katika kikosi hicho cha Stamford Bridge uliomfanya ashinde tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu wa klabu, kocha wa Brazil, Carlo Ancelotti alimuacha Pedro nje ya kikosi chake cha wachezaji 26 kwa ajili ya mashindano hayo, huku akimjumuisha Neymar.
Maumivu ya kuachwa kwake yalionekana baada ya video kusambaa zikionyesha familia na marafiki wa Pedro waliokusanyika Sao Paulo kuanza kurusha vijembe na kejeli dhidi ya Neymar, licha ya staa huyo wa Chelsea kumshukuru Ancelotti kwa kikosi alichokitangaza.
Katika eneo la Ribeirao Preto marafiki wa Pedro walichoma nyama na kupamba nyumba yake kwa rangi za kijani na njano zinazotambulika kuwa za timu ya taifa ya Brazil, tukio ambalo lilikwenda sambamba na maneno ya kuukejeli uteuzi wa Neymar.
“Tunasikitika sana kwa sababu tunajua huu ni ndoto yake,” alisema mchezaji wa zamani Jimmy Barboza, rafiki wa karibu wa Pedro.
“Kila wakati tunatarajia aitwe kwenye kila mechi. Bahati mbaya safari hii haikuwa hivyo. Sasa tunapaswa kuiunga mkono Brazil. Nitamtumia ujumbe. Ni jambo la kushangaza. Sijui kama Ancelotti tayari amezungumza naye au la, lakini sisi kama marafiki tutafanya sehemu yetu.”
Arthur Mendonca, rafiki wa Pedro tangu utotoni alisisitiza kuwa nyota huyo wa Chelsea alistahili zaidi nafasi katika kikosi hicho kuliko baadhi ya walioteuliwa na Ancelotti, ingawa hakutaja majina.
“Alikuwa na nafasi kubwa ya kwenda. Niliamini angeitwa, hasa kutokana na muda na kiwango chake. Ukilinganisha na wengine, alikuwa kwenye kiwango bora zaidi. Kuna mitazamo tofauti na Neymar hakustahili hata kama jina lake ni kubwa, kwani kafanya nini?”
Vanessa Barbosa, rafiki wa familia, alisema anaamini Pedro ataweza kushinda maumivu ya kutochaguliwa.
“Inakatisha tamaa. Hilo ndilo pekee naweza kusema. Lakini Joao Pedro ni kijana mwenye tabia bora. Ana ukomavu mkubwa kwa umri wake na nina uhakika atapita kipindi hiki. Bila shaka ana huzuni, lakini jambo hili halitamtikisa. Chochote kitakachotokea, tupo pamoja naye,” alisema.