Habari za michezo

GHETO KIDS KUTUMBUIZA NA SHAKIRA KOMBE LA DUNIA 2026

Vardo May 20, 2026 10:10 pm

Kundi maarufu la watoto wanaocheza muziki kutoka Uganda, Ghetto Kids, limepata nafasi kubwa ya kimataifa baada ya kualikwa na staa wa muziki kutoka Colombia, Shakira kushiriki kwenye burudani ya mapumziko katika mechi ya fainali ya Kombe la Dunia 2026.

Shakira ametangaza taarifa hiyo Jumatano Mei 20, 2026 kupitia video aliyoiweka kwenye ukurasa wake rasmi wa Instagram wenye wafuasi zaidi ya milioni 95 wakati akizungumza kuhusu wimbo rasmi wa mashindano hayo uitwao ‘Dai Dai’ alioufanya kwa kushirikiana na msanii wa Nigeria, Burna Boy.

Katika video hiyo, Shakira amesema amevutiwa na jinsi mashabiki duniani walivyoupokea wimbo huo huku video nyingi za watu wakicheza zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii.

“Nimeshawaalika Ghetto Kids kutoka Uganda,” amesema Shakira huku akilitaja kundi hilo kama sehemu ya wabunifu wa kimataifa walioufanya wimbo huo kuteka dunia kupitia dansi zao.

Michuano ya Kombe la Dunia 2026 itafanyika kuanzia Juni 11, 2026 hadi Julai 19, 2026 katika miji 16 ya Marekani, Mexico na Canada.

Ghetto Kids ilianzishwa mwaka 2014 na Dauda Kavuma, ikiwa ni kundi la watoto kutoka mitaa ya Katwe jijini Kampala nchini Uganda.

Kundi hilo lilianza kujulikana kimataifa baada ya video yao ya kucheza wimbo wa ‘Sitya Loss’ wa Eddy Kenzo kusambaa kwa kasi mtandaoni.

Tangu hapo, Ghetto Kids wameonekana kwenye majukwaa mbalimbali makubwa duniani ikiwemo video ya wimbo wa ‘Unforgettable’ ya French Montana pamoja na matukio yaliyohusiana na Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.

Mwaka 2023 kundi hilo pia lilipata Golden Buzzer kwenye mashindano ya Britain’s Got Talent, jambo lililoendelea kuliimarisha kama moja ya makundi makubwa ya watoto wanaocheza muziki barani Afrika.

CHILUNDA AIBEBA TRA UNITED IKILIPA KISASI KWA MTIBWA