Habari za michezo
CLARA LUVANGA ANG’ARA TENA SAUDIA
Vardo
May 21, 2026
11:00 pm
NYOTA wa kimataifa wa Tanzania, Clara Luvanga ameendelea kukiwasha Saudi Arabia baada ya kuiongoza Al Nassr ya Wanawake kutwaa ubingwa wa Kombe la SAFF Women’s Cup kwa ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya watani wao wa jadi, Al Hilal katika fainali iliyopigwa Kingdom Arena.
Katika mechi hiyo iliyokuwa na ushindani mkubwa kwa timu zote mbili, Clara aliandika historia nyingine baada ya kufunga mabao yote matatu ya Al Nassr dakika ya 86, 96 na 107, akiiwezesha timu hiyo kuibuka mabingwa baada ya mechi hiyo kwenda dakika 120 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 za kawaida.
Hat-trick hiyo ya fainali imezidi kuthibitisha ubora wa mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga Princess ambaye sasa ameendelea kuwa tegemeo kubwa katika kikosi hicho.
Clara pia alikabidhiwa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mashindano (MVP) kutokana na kiwango chake bora alichokionyesha katika michuano hiyo iliyomalizika usiku wa Mei 20, 2026.
Mshambuliaji huyo alimaliza mashindano hayo akifunga mabao saba, bao moja nyuma ya mshambuliaji nyota wa Nigeria, Asisat Oshoala aliyemaliza na mabao manane na kutwaa tuzo ya mfungaji bora wa mashindano hayo.
Licha ya kukosa kiatu cha ufungaji bora kwa tofauti ya bao moja, Clara ameendelea kuthibitisha ubora wake wa kufumania nyavu baada ya kufanya vizuri kwenye ligi alipofunga mabao 24 na kuisaidia Al Nassr kutwaa ubingwa wa ligi kwa mara nyingine.
Msimu huu ameweka rekodi ya kubeba mataji mawili mfululizo akiwa na Al Nassr, likiwemo la ligi na sasa SAFF Women’s Cup lakini ukiwa ubingwa wa nne kwa nyota huyo tangu ajiunge nao msimu wa 2023-2024 akitokea Dux Lugrono ya Hispania.
Hat-trick ya fainali haikuwa mara ya kwanza kwa nyota huyo kuwatesa Al Hilal, kwani Machi 26 mwaka huu alifunga mabao matatu katika ushindi wa 4-1 wa dhidi ya mahasimu hao kwenye mechi ya ligi kuu iliyowapa ubingwa.
Kwa mujibu wa takwimu za ligi hiyo, Al Nassr sasa imetwaa ubingwa wa ligi kwa mara ya nne mfululizo, huku huu ukiwa msimu wa tatu mfululizo kwa Clara kushuhudia mafanikio hayo tangu ajiunge na timu hiyo.
Msimu wake wa kwanza Al Nassr alifunga mabao 11 na asisti saba kwenye mechi 12, msimu wa 2024-2025 alimaliza na mabao 21 na asisti saba kwenye mechi 14 na huu akimaliza mfungaji bora akiweka kambani mabao 24 na asisti tatu kwenye mechi 14.
Akizungumzia ubingwa huo, Clara amesema: “Kwanza ni furaha kubwa sana kwangu kutimiza malengo ya timu msimu huu lakini pia mwanzoni mwa msimu nilidhamiria kuhakikisha nabeba kiatu nashukuru nimechuku kwenye ligi.”