Chama Simba
Simba SC

EDO KUMWEMBE:- MPAKA SASA CHAMA 2, SIMBA 1….YANGA WANAJIFICHA KWA AIBU….

admin May 25, 2026 6:16 pm

GHAFLA kila kitu kimebadilika kwa Clatous Chota Chama. Alirudi zake Simba akiwa mnyonge. Mambo mawili. Kwanza kabisa ilionekana kama vile msaliti amerudi kundini. Kitendo cha kwenda Yanga kiliwasononesha mashabiki wengi wa Simba.

Alirudi zake Simba na alipokelewa kwa sababu timu haikupata mbadala wake. Ubunifu katika eneo la mbele la Simba ulipungua. Mchezaji kama Josh Mutale asingeweza kuwapeleka Simba katika nchi ya Ahadi.

Awali kulikuwa na mgawanyiko wa mawazo kutoka kwa viongozi. Kuna ambao hawakutaka kumwona tena Chama akivaa jezi nyekundu na nyeupe. Kwenda Yanga iliwaumiza kwa kiasi kikubwa. Lilikuwa teke la mdomoni.

Kabla hata hajaenda Yanga alionekana mchezaji msumbufu. Kuna Kundi ambalo aliwahi kuwekwa pamoja na Aishi Manula, walikuwa wanaihujumu timu hasa kwa wapinzani wao Yanga.

Kitendo cha kwenda Yanga kilichukuliwa kama hitimisho la mawazo yao, labda alikuwa kweli ‘anawauza’ wakati akiwa anavaa jezi yao. Hata hivyo, kwa namna Simba walivyopitia magumu hapa katikati nadhani watu waliokuwa wanataka arudi, walishinda kura ya veto katika vikao.

Chama alirudi Simba kinyonge pia kwa sababu ilionekana kama zama zake zimepita. Simba wenyewe walimpa mkataba wa mwaka mmoja wakiashiria kutomwamini moja kwa moja. Lakini ghafla kila kitu kimebadilika tena.

Chama amerudi zake katika timu na amerudisha ufalme wake. Ameichukua timu ameitia mfukoni kwake. Mechi dhidi ya mtani alipika bao la kwanza la Libasse Gueye, lakini akafunga la kushangaza ambalo hata wazungu huko mbele walilishangaa.

Kuanzia hapo amekuwa akifunga au akipika mabao na kuwa mchezaji bora wa mechi. Na sasa imethibitika ni bora uwe na Chama mwenye umri wa miaka 34 kuliko kuwa na Joshua Mutale mwenye umri wa miaka 23.

Bora upate ubora wa asilimia 40 tu kutoka kwa Chama kuliko kuwa na mchezaji mwingine katika nafasi yake na sasa amerudisha heshima yake kwanza kabisa katika mpira wetu, pia amerudisha heshima kwa mashabiki wa Simba.

Jinsi alivyo mjanja ni wazi tupo mwezi Mei na ifikapo mwisho wa msimu ni ndiye atakayekuwa anatembea na mkataba wake mkononi. Mabao yake na kiwango chake vinarudisha nguvu yake ya majadiliano katika mkataba mpya. Chama alidhalilika sana kiasi cha kwenda kucheza Singida Black Stars.

Kwa sasa anaweza kuamua kuweka kigingi cha kutaka mkataba wa miaka miwili klabuni. Sidhani kama kutakuwa na kiongozi ambaye atakuwa na ubavu wa kumbishia. Kiongozi huyo ataeleweka vipi kwa mashabiki?

Walau pia amerudisha nguvu ya kutaka dau kubwa la kusaini mkataba mpya. Wakati anarudi Simba hakuwa na nguvu hiyo kwa sababu mbili. Kwanza kabisa ilionekana anahiitaji Simba kuliko ilivyomhitaji.

Ni wazi Simba walikuwa katika nafasi nzuri katika mazungumzo kuliko Chama. Uswahilini tunasema Simba walikuwa wameshika mpini na na Chama alikuwa ameshika makali. Kwa sasa kibao kinaelekea kugeuka kwa kasi.

Mwisho wa msimu atakuwa katika nafasi nzuri ya kuingia katika ofisi za Simba akitembea kifua mbele. Ni heshima ambayo anastahili. Heshima ambayo amejitengenezea kwa muda mfupi tu.

Yanga wanajisikiaje kuhusu Chama? Huwa inatokea. Walimchukulia poa kwa sababu walikuwa na wachezaji wengi wazuri kwa wakati ule. Hawakumtumia Chama vyema na ilionekana kama wamemdhalilisha.

Kuna wachezaji wanacheza vizuri zaidi wakiwa wanaaminiwa. Kuna wachezaji wanacheza vizuri zaidi wakiwa wanathaminiwa. Chama anajihisi kuthaminiwa na kuaminiwa zaidi Simba na ndiyo maana anawafanyia mambo makubwa. Yanga hawakuwahi kumpa thamani hiyo.

Wanajuta? Sina uhakika sana kwa sababu bado wana timu nzuri. Bila ya ujio wa Alain Okello nadhani wangekuwa wamejivua nguo zaidi kwa sababu Pacome Zouzoua haonekani kuwa katika kiwango bora kama alivyokuwa miaka ya karibuni. Uzuri ni Okello amewavalisha nguo katika wakati sahihi.

Hata hivyo, lazima kutakuwa na kundi la mashabiki ambao wanajuta kwa kutoendelea kuwa na Chama. Na kilichowaudhi zaidi ni namna alivyofanya mambo makubwa katika pambano dhidi yao. Kibinadamu lazima uumie. Na kibinadamu ni lazima Chama alifurahi zaidi kwa sababu anahisi Yanga walimdhalilisha na kumpotezea muda kwa kumfanya atumie muda mwingi akiwa amesota benchi.

CHAMA KUPEWA URAIA

Rafiki yangu mheshimiwa sana, Paul Makonda, Waziri wa habari, sanaa, utamaduni na michezo majuzi alisikika akidai alikuwa na wazo la kumpa Chama uraia. Nadhani mheshimiwa alikuwa anafurahisha genge tu.

Chama anaweza kupewa uraia kama mgeni mwingine yeyote yule lakini hawezi kuichezea timu ya taifa kwa sababu tayari ameichezea timu yake ya taifa ya Zambia mechi nyingi. Anaweza kupewa kama mzawa ambaye amekaa nchini kwa miaka mingi lakini kwa sasa hana hadhi ya kuichezea timu ya taifa kwa mujibu wa kanuni za FIFA.

Credit:- Edo Kumwembe/MwanaSpoti

NAMUNGO KIBARUA KIGUMU KMC COMPLEX, YANGA HAKUNA MCHEZO WA KUBEZA SKAUTI WA FIFA AGOMA KUSEPA TZ KISA ‘MAVITU’ YA OKELLO…KAULI YAKE HII HAPA…