Michezo

NAMUNGO KIBARUA KIGUMU KMC COMPLEX, YANGA HAKUNA MCHEZO WA KUBEZA

Vardo May 25, 2026 4:07 pm

NYASI za Uwanja wa KMC Complex leo zinatarajiwa kuwa na moto wa aina yake, ambapo Yanga SC watawaalika Namungo FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ukiwa na uzito mkubwa kwa upande wa vinara wa msimamo.

Yanga wanaingia uwanjani wakiwa na dhamira moja tu,kupata ushindi ili kurejea kileleni mwa ligi, baada ya kushushwa na wapinzani wao wa jadi Simba SC waliowapita kwa tofauti ya pointi moja.

Hivi sasa Simba wanaongoza wakiwa na pointi 58, huku Yanga wakiwa nafasi ya pili kwa pointi 57, hivyo mchezo wa leo ni zaidi ya mechi ya kawaida.

Kuelekea mtanange huo, kaimu kocha mkuu wa Yanga, Abdihamid Moallin, amesisitiza kuwa kikosi chake kipo tayari kwa kila hali, kiwiliwili na kiakili, kuhakikisha kinapata matokeo chanya mbele ya Namungo.

Moallin amesema presha iliyopo kwenye mbio za ubingwa si kitu kinachowatisha, bali ni sehemu ya maisha ya Yanga kama klabu kubwa inayocheza kila mechi kwa malengo makubwa.

“Tunatambua umuhimu wa kila mchezo, hatuogopi kufanya kazi katika mazingira yenye presha. Tunacheza kama tunavyocheza siku zote, sisi ni Yanga. Presha inatufanya tuzidi kuwa bora zaidi,” amesema.

Ameongeza kuwa malengo yao ni wazi kabisa—kuondoka KMC Complex wakiwa na pointi tatu muhimu, bila kujali ubora au historia ya mpinzani wanaokutana naye.

“Kila mchezaji anajua matarajio ya mashabiki na klabu. Tunataka kila mmoja aingie uwanjani akiwa tayari kupambana kwa asilimia 100. Hakuna mchezo wa kubeza,” ameongeza.

Pia ametoa taarifa njema kwa mashabiki kuhusu hali ya kikosi, akibainisha kuwa wachezaji wengi wako fiti, huku kiungo Pacome Zouzoua akionyesha nafuu baada ya majeraha madogo aliyoyapata mchezo uliopita.

Moallin amehitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa sapoti ya mashabiki, akiwataka Wanayanga kujitokeza kwa wingi uwanjani ili kuongeza nguvu ya ushindi.

“Namungo ni timu ngumu na inahitaji heshima, lakini hilo halibadili malengo yetu. Tunajiandaa kushinda kila mchezo, na leo haitakuwa tofauti,” alisema.

NZENGELI AFICHUAA SIRI YA MBIO ZA MABAO, FEI TOTO AWAACHA WENGINE MBALI