Yanga SC

ZIMBWE JR AFICHUA SIRI YA YANGA KUTIKISA LIGI

Vardo May 27, 2026 4:39 pm

BEKI wa Yanga SC, Mohammed Hussein ‘Zimbwe Jr’, amesema kikosi hicho kina kila sababu ya kuwa na matumaini makubwa ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu kutokana na kiwango bora kinachoendelea kuonyeshwa katika hatua za mwisho za msimu.

Kwa sasa Yanga inaongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 60, huku watani wao wa jadi, Simba SC, wakifuatia kwa pointi 58 pekee. Tofauti hiyo ya alama mbili imeendelea kuongeza presha na ushindani mkubwa katika mbio za ubingwa zinazozidi kupamba moto kila wiki.

 

Licha ya ushindani huo kuwa mkali, Zimbwe Jr anaamini Yanga bado ipo kwenye nafasi nzuri zaidi ya kubeba taji kutokana na uimara wa kikosi hicho na namna wachezaji wanavyoendelea kujitoa kwa asilimia mia moja ndani ya uwanja.

 

Beki huyo amesema siri kubwa ya mafanikio yao ni mwendelezo wa kiwango kizuri cha timu, huku kila mchezaji akiwa na ari ya kupambana hadi dakika ya mwisho bila kukata tamaa.

“Mbio za ubingwa bado ziko wazi, lakini nafasi kubwa tunayo sisi Yanga kwa sababu tupo juu kwa alama mbili.

Tunaendelea vizuri na ukiangalia ubora wa timu kila siku unazidi kupanda. Nina imani hadi mwisho wa msimu tutakuwa mabingwa,” amesema Zimbwe Jr.

Nyota huyo ameongeza kuwa morali kubwa waliyonayo wachezaji kambini ndiyo inayowapa jeuri ya kuendelea kuamini katika safari yao ya kutetea ubingwa huo, hasa kutokana na namna timu inavyocheza kwa kujituma kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho.

“Kikubwa kinachonipa ushujaa ni namna timu yetu inavyopambana kwa nguvu zote ndani ya dakika 90. Wachezaji wote wana ari kubwa ya ushindi na hilo linaifanya Yanga kuwa timu ngumu sana kwa sasa,” amesema beki huyo wa Yanga.

UBINGWA KWENDA KWA NANI LEO……….? MOALLIN FUNGUKA SIRI YA YANGA KUTWAA TENA UBINGWA