Michezo Bongo

COASTAL IJIANDAE NA MAISHA BILA HAWA WATATU

Vardo May 28, 2026 11:55 pm

KIJIWE chetu kinafahamu vyema historia ya Coastal Union hasa linapofika suala la kuuza wachezaji kwenda timu nyingine.

Coastal Union siyo timu ambayo huwa inabania wachezaji pindi wanapopata maslahi bora kwingine na badala yake huwapa baraka wakavune noti kwingine.

Mfano wa hivi karibuni ni wachezaji kama Lameck Lawi, Abdul Sopu, Bakari Mwamnyeto na Victor Akpani ambao Wagosi wa Kaya ilikubali kuwauza katika timu za Azam, Yanga na Simba.

Sasa tukikitazama kikosi cha sasa hivi cha Coastal Union, kuna wachezaji watatu ambao kiwango bora wanachokionyesha kinaweza kuwapa malisho bora zaidi katika dirisha kubwa la usajili hivyo timu hiyo ya Tanga bora ianze kujiandaa kisaikolojia kutafuta warithi wao.

Wawili ni viungo wakabaji ambao wote kwa mechi tofauti wamekuwa wakivaa kitambaa cha unahodha cha Coastal Union ambao ni Greyson Gwalala na Geofrey Manyasi.

Viungo hasa katika kuilinda safu ya ulinzi ya Coastal Union, wazuri katika kupokonya mipira, kuchezesha timu na kuziunganisha safu za ulinzi na ushambuliaji.

Halafu kuna mshambuliaji Bakari Msimu. Tishio sana pale mbele. Ana kasi, akili ya mpira na uamuzi wa haraka pindi anapokuwa na mali mguuni jambo linalomfanya awe mwiba kwa walinzi wa timu pinzani. Hao watatu siku ukiwakuta wakiwa katika ubora wao, usitegemee kama utapata mechi nyepesi na rahisi dhidi ya Coastal Union na nadhani macho ya timu nyingi yanawatamani kwa sasa. Ni wachezaji ambao wanadhihirisha kwamba jicho la Coastal Union katika kutazama na kushawishika na vipaji vya wachezaji, linafanya kazi.

MERIDIANBET YAMLETA PET KUIPANDISHA THAMANI MICHEZO NANI KUUNGANA NA YANGA, SIMBA CAF