NANI KUUNGANA NA YANGA, SIMBA CAF
Wakati Ligi Kuu ikiwa katika mapumziko ya wiki mbili kupisha michezo ya kalenda ya Fifa na timu za Taifa, hadi Yanga na Simba zimefuzu kushiriki mashindano ya CAF, lakini bado hazijajua ni mashindano gani kati ya Ligi ya Mabingwa au Kombe la Shirikisho zitashiriki msimu ujao.
Hii inatokana na nafasi ya Azam FC ambayo kwa mujibu wa msimamo wa sasa, inaweza kuzipiku Yanga na Simba kwa idadi ya pointi na kupindua meza.
Mpaka sasa, kila timu imebakiza mechi tano, huku mabingwa watetezi Yanga wakiwa kileleni kwa pointi 60 na Simba wakifuatia kwa pointi 58.
Azam FC wanashika nafasi ya tatu kwa pointi 52 na endapo itashinda mechi zote zilizobakia watafikisha pointi 67.
Timu hiyo inaweza kutwaa ubingwa au kumaliza nafasi ya pili endapo Yanga na Simba zitafanya vibaya katika michezo yao iliyobakia.
Endapo hali itakuwa hivyo, Azam FC inaweza kuwa bingwa na hivyo kuiwakilisha nchi katika mashinano ya ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa upande wa Yanga, mpaka sasa bado hawaja jihakikishia kushiriki katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwani Azam FC inaweza kuzifikia na vile vile kuzipiku pointi zake ikiwa itashinda mechi zake zilizosalia.
Yanga itafikisha pointi 75 ikiwa itashinda mechi zote zilizobakia na hivyo kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara na kufuzu moja kwa moja katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa upande wa Simba, wanaweza kufikisha pointi 73 kama watashinda mech zale zote zilizobaki na kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika pia.
Mpaka sasa, Yanga wanahitaji pointi nane zaidi ili kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati Simba wanahitaji pointi 10 kuhakikisha wanatinga michuano hiyo mikubwa barani Afrika na Azam FC, wanahitaji pointi nne pekee kuthibitisha nafasi ya kushiriki mashindano ya CAF msimu ujao mbele ya Singida Black Stars.
Hali hiyo inatokana na uwiano wa matokeo ya Azam FC na Singida Black Stars zilipokutana ambapo Azam FC imeshinda mechi moja na kutoka sare pia. Singida Black Stars mpaka sasa inaweza kufikisha pointi 56 endapo itashinda mechi zote.
Endapo Singida Black Stars itashinda mechi zote zilizosalia, itakuwa imeziondoa timu za JKT Tanzania na TRA United FC ambazo hazitaweza kufikia pointi hizo. JKT Tanzania wanaweza kumaliza msimu wakiwa na pointi 53 pekee, huku TRA United wakifikisha pointi 52.
Kwa hali ilivyo katika msimamo wa sasa, Yanga, Simba na Azam FC tayari zimekata tiketi ya kushiriki mashindano ya CAF na vita inabaki kwa timu tatu, Singida Black Stars, JKT Tanzania na TRA United.
Kwa mujibu wa kanuni, timu mbili za juu katika Ligi Kuu Bara hufuzu kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, huku mshindi wa Kombe la Shirikisho la CRDB pamoja na timu itakayomaliza katika nafasi ya tatu zitakata tiketi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Wakati huo huo, kwa upande kombe la Shirikisho, timu ya Coastal Union ina nafasi ya kushiriki katika mashindano hayo endapo itatwaa ubingwa.
Mpaka sasa, Coastal Union ni miongoni mwa timu nne zilizofuzu hatua ya nusu fainali ya kombe la Shirikisho la CRDB. Timu nyingine ni Yanga, Simba na Azam FC.
Endapo Coastal Union itatwaa ubingwa wa kombe hilo, itakuwa imekata rasmi tiketi ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya Shirikisho ya CAF huku ikihitimisha safari za Singida, JKT Tanzania na TRA United.