Singida Big Stars FC

WATATU WAINGIA RADA ZA SINGIDA BLACK STARS

Vardo May 29, 2026 9:16 am

MABOSI wa Singida Black Stars wameanza mchakato wa kimya kimya wa kukisuka kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao, ambapo kwa sasa inaangalia uwezekano wa kusajili wachezaji watatu wazawa, kwa lengo la kuboresha timu hiyo.

Nyota wanaowindwa na timu hiyo ni kipa, Yona Amos wa Pamba Jiji wenye Clean Sheets saba za Ligi Kuu Bara, ambaye mara kadhaa alikuwa akihusishwa na miamba wa soka nchini wa Yanga na Simba.

Yona aliyekuwa akihusishwa mara kadhaa kujiunga na Yanga na Simba tangu akiwa na maafande wa Tanzania Prisons, anapewa nafasi zaidi ya kusajiliwa Singida Black Stars, ili akaongezee nguvu eneo hilo baada ya makipa wao wa sasa Metacha Mnata na Amasi Obasi kuonyesha mapungufu katika msimu huu.

Kipa Amos anamaliza mkataba wake na Pamba Jiji mwishoni mwa msimu huu wa 2025-2026, ambapo tayari Singida imeonyesha nia ya kumhitaji kwa ajili ya kupata saini yake, kwa lengo la kukiboresha kikosi hicho ili kilete ushindani kwa msimu ujao.

Mbali na Yona, uongozi wa Singida unamfuatilia kwa ukaribu beki wa kati wa Mtibwa Sugar, Haroun Lyawatwa ambaye amekuwa muhimili mkubwa tangu akiwa na kikosi cha vijana cha timu hiyo, hadi sasa anapoendelea kuichezea ya wakubwa kikosini.

Lyawatwa aliyefunga bao moja la Ligi Kuu Bara msimu huu amekuwa na kiwango bora, jambo lililowaibua mabosi wa Singida kuanza kuifuatilia saini yake.

Nyota wengine mzawa anayewindwa Singida, ni kiungo mshambuliaji wa Coastal Union, Bakari Msimu ambaye tayari inaelezwa uongozi wa Simba pia unaangalia uwezekano wa kuipata saini yake, kutokana na kuridhishwa na kiwango chake anachoonyesha.

Msimu aliyeifungia Coastal Union mabao matatu ya Ligi Kuu Bara msimu huu hadi sasa, tayari amekuwa ni miongoni mwa nyota wanaoangaliwa na timu tofauti msimu ujao, kutokana na kiwango bora anachoonyesha, ikiwa ataachana na ‘Wagosi wa Kaya’.

Chanzo kutoka Singida, kililiambia Mwanaspoti wachezaji wote watatu kwa maana ya Yona Amos, Haroun Lyawatwa na Bakari Msimu ni miongoni mwa nyota wanaowafuatilia kwa ajili ya kupata saini zao kwa msimu ujao, japo mazungumzo yanaendelea.

“Malengo yetu msimu ujao ni kusajili wachezaji watatu hadi wanne tu wazawa, hatutakuwa na maingizo mapya kwa sababu wapo wa kigeni tutakaokuwa nao, tunaendelea na mchakato na tuko katika mwelekeo mzuri wa kufanikisha,” kimesema chanzo hicho.

NANI KUUNGANA NA YANGA, SIMBA CAF AMANI JOSIAH, MINZIRO KAZI ZINAZUNGUMZA