AZIZ KI AITIKISA YANGA KWA KAULI YA KUREJEA TANZANIA
WAKATI tetesi za usajili zikizidi kushika kasi kuelekea dirisha lijalo la usajili, kiungo mshambuliaji wa Ittihad SC ya Libya, Stephane Aziz Ki ameibua gumzo baada ya kufunguka kuhusu uwezekano wa kurejea tena ndani ya kikosi cha Yanga.
Aziz Ki, ambaye aliwahi kuwa mmoja wa nyota muhimu wa Yanga kabla ya kuondoka mwanzoni mwa mwaka huu, amesema bado mlango uko wazi kwake kurejea Tanzania siku zijazo na kuivaa tena jezi ya timu hiyo iliyompa umaarufu mkubwa barani Afrika.
“Inshallah huwezi kujua. Naweza kurejea Tanzania na kucheza tena ndani ya kikosi cha Yanga,” amesema Aziz Ki.
Kauli hiyo imeongeza nguvu ya taarifa zinazoeleza kuwa Yanga tayari wameanza kufanya maandalizi ya kumrudisha nyota huyo, huku ikidaiwa kuwa mabosi wa klabu hiyo wanafuatilia kwa karibu mazingira ya kumpata tena kiungo huyo mwenye uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi na kufunga mabao.
Taarifa zinaeleza kuwa Aziz Ki mwenyewe anatamani kurejea Yanga, jambo ambalo limeifanya klabu hiyo kuanza mchakato wa awali wa kutuma ofa rasmi kwa Al-Ittihad SC muda wowote kuanzia sasa.
Nyota huyo wa Burkina Faso alijiunga na Al Ittihad mwezi Januari mwaka huu kwa mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya dola 400,000 za Marekani, sawa na zaidi ya Sh bilioni 1 za Kitanzania.
Hata hivyo, kutokana na mahusiano mazuri aliyowahi kuwa nayo ndani ya Yanga pamoja na mapenzi makubwa kutoka kwa mashabiki wa klabu hiyo, uwezekano wa kurejea kwake umeanza kuonekana kuwa mkubwa kadri siku zinavyosogea.