YANGA HAWAFANYI MAKOSA, MAX NZENGELI AWEKA WAZI MSIMAMO
KIUNGO wa Yanga SC, Max Nzengeli, amesema kikosi hicho kinaendelea kupambana kwa nguvu kuhakikisha kinapata ushindi katika kila mchezo huku mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara zikizidi kupamba moto kuelekea mwisho wa msimu.
Nzengeli amesema ndani ya kikosi hicho kwa sasa msisitizo mkubwa haupo katika kuwaangalia wapinzani wao wa karibu, bali kuhakikisha wanatimiza malengo yao ya kushinda mechi zote zilizobaki ili kuendelea kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa.
“Hatupambani sana na mpinzani wetu bali tunahitaji kushinda na kuendelea kusaka ushindi. Haijakuwa rahisi na haitakuwa rahisi, lakini tunapambana kushinda kila mechi yetu,” amesema Max.
Kauli hiyo inaonyesha namna wachezaji wa Yanga walivyojipanga kuhakikisha hawapotezi mwelekeo katika kipindi hiki muhimu cha msimu, ambapo kila pointi imekuwa na uzito mkubwa kwenye vita ya ubingwa.
Nyota huyo ameongeza kuwa ushindani wa ligi msimu huu umeongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na timu nyingi kuimarika, jambo linalofanya kila mchezo kuwa mgumu na wenye ushindani mkubwa ndani ya dakika 90.
Licha ya changamoto hiyo, Yanga imeendelea kuonyesha morali kubwa ya kupambana hadi mwisho wa msimu, huku mashabiki wa timu hiyo wakibaki na matumaini makubwa ya kuona kikosi chao kikimaliza msimu kwa mafanikio na kutwaa taji la ligi.