WENGER ASEMA SERENGETI BOYS NI MUSTAKABALI MPYA WA SOKA AFRIKA
ALIYEKUWA kocha mkuu wa Arsenal, Arsène Wenger, ameipongeza Tanzania kufuatia mafanikio ya timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys, kufuzu kucheza fainali ya michuano ya AFCON U17 inayoendelea nchini Morocco.
Wenger amesema hatua hiyo ni ishara kubwa ya maendeleo ya soka la vijana Tanzania, huku akieleza kuwa ushindani na nidhamu waliyoionyesha Serengeti Boys ni jambo la kujivunia kwa bara la Afrika.
Serengeti Boys ilitinga hatua ya fainali baada ya kuiondosha Egypt kwa ushindi wa mikwaju ya penalti 4-3, kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90 za mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa.
Katika mchezo huo, vijana wa Tanzania walionyesha uimara mkubwa wa safu ya ulinzi pamoja na utulivu wa kipa wao, hali iliyowafanya kuwazuia Wamisri kupata bao lolote kabla ya ushindi kupatikana kupitia changamoto ya penalti.
Ushindi huo umeendelea kuamsha furaha kubwa kwa mashabiki wa soka Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla, huku wengi wakiamini kizazi hicho kinaweza kuwa msingi imara wa mafanikio ya soka la taifa siku zijazo.
Sasa Serengeti Boys inajiandaa kuivaa Senegal katika mchezo wa fainali wa AFCON U17 utakaopigwa Juni 2 nchini Morocco, ambapo Tanzania itakuwa ikisaka kuandika historia mpya kwa kutwaa ubingwa huo wa vijana barani Afrika.