Simba SC

SIMBA YAWEKA REKODI KALI, BARKER AENDELEA KUNG’ARA

Vardo May 29, 2026 8:54 pm

KOCHA Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, anaendelea kuweka rekodi ya kuvutia ndani ya klabu hiyo baada ya kuiongoza timu kucheza michezo 27 mfululizo bila kupoteza katika mashindano mbalimbali msimu huu.

Chini ya Barker, Simba imeonyesha uimara mkubwa na mwendelezo wa kiwango bora, hali inayowafanya wabaki kuwa miongoni mwa timu zinazotoa presha kubwa katika mbio za ubingwa. Katika mechi hizo, Simba imefanikiwa kushinda michezo 13 na kutoka sare saba kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

 

Mbali na mafanikio hayo ya ligi, Simba pia imeendelea kufanya vizuri katika michuano mingine, ikishinda mechi nne za Kombe la Shirikisho la CRDB Bank pamoja na michezo mitatu ya Kombe la Muungano, jambo linalodhihirisha ubora wa kikosi hicho katika mashindano tofauti.

Mfululizo huo wa matokeo mazuri umeongeza matumaini makubwa kwa mashabiki wa Simba ambao wanaamini timu yao ipo kwenye njia sahihi ya kumaliza msimu kwa mafanikio makubwa. Uwezo wa timu kupambana katika kila mchezo umeonekana kuwa moja ya silaha kubwa chini ya Barker.

Kocha huyo pia amepewa sifa kwa kujenga kikosi chenye nidhamu, kujiamini na mshikamano mkubwa uwanjani. Utulivu wa benchi la ufundi pamoja na ubora wa wachezaji umeendelea kuwa msingi muhimu wa mafanikio ya Simba katika kipindi hiki cha mwisho wa msimu.

Kauli mbiu ya “One Game at a Time” imeendelea kuonekana kuwa sehemu ya falsafa ya Simba chini ya Barker, huku kila mchezo ukipewa uzito mkubwa bila kuangalia presha ya mbio za mataji.

Kadri msimu unavyozidi kuelekea tamati, macho ya wengi sasa yanaelekezwa kwa Simba kuona kama itaweza kuendeleza rekodi hiyo ya kutopoteza na hatimaye kutwaa mataji muhimu chini ya kocha Steve Barker.

SERENGETI BOYS YAFUNGUA MLANGO WA DUNIA, TANZANIA YAANZA KUOGOPWA RATIBA YAMUIBUA KOCHA MUEMBE MAKUMBI