SERENGETI BOYS YAFUNGUA MLANGO WA DUNIA, TANZANIA YAANZA KUOGOPWA
USHINDI wa Serengeti Boys dhidi ya Misri umeendelea kuibua matumaini makubwa kwa timu hiyo ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, baada ya Kocha Mkuu Elieneza Nsangazelu kusema kuwa matokeo hayo ni uthibitisho wa uwezo mkubwa walionao kuelekea hatua zinazofuata za kimataifa.
Serengeti Boys ilifanikiwa kutinga fainali baada ya kuiondoa Misri kwa mikwaju ya penalti 4-3, kufuatia dakika 90 za mchezo mgumu uliomalizika kwa sare tasa. Mechi hiyo ilishuhudia ushindani mkubwa, kila upande ukionekana kusaka nafasi ya kuandika historia.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Nsangazelu amesema ushindi huo umewapa nguvu mpya na kuongeza imani ndani ya kikosi chake kwamba hakuna jambo lisilowezekana wanapokuwa na umoja, nidhamu na kujituma.
“Ushindi huu umetupa imani kwamba hakuna jambo linaloshindikana. Tumeweza kufanya hapa na tunaweza kufanya hata zaidi huko mbele tunakoelekea,” amesema kocha huyo.
Nsangazelu amesisitiza kuwa macho yao sasa yameelekezwa kwenye michuano ya Kombe la Dunia kwa vijana, ambapo anaamini kikosi hicho hakitakwenda kushiriki tu, bali kupambana kwa malengo makubwa ya kufanya vizuri na kuiwakilisha vyema Tanzania.
“Watanzania wajiandae kwa sababu hatutaenda kinyonge. Tutaenda kama wachezaji wakubwa wenye malengo ya kufanya vizuri na kuipeperusha vyema bendera ya taifa,” ameongeza.
Amewapongeza wachezaji wake kwa nidhamu, moyo wa kujituma na umoja waliouonesha katika mashindano hayo, akiwataka Watanzania kuendelea kuwaunga mkono kwani safari bado ni ndefu na inahitaji sapoti ya kila mmoja.
Nsangazelu amesema anaamini kuwa kwa msaada wa Mungu na mshikamano wa Watanzania wote, Serengeti Boys ina uwezo wa kwenda mbali zaidi na kuandika historia mpya katika soka la vijana.