SINGIDA BS YAWEKEWA SH50 MIL KWA MBAPPE
UONGOZI wa Singida Black Stars umeanza rasmi mazungumzo ya kumpata mshambuliaji wa Mlandege FC ya Zanzibar, Mussa Hassan Simba ‘Mbappe’ kwa ajili ya kuongeza nguvu eneo hilo, japo itapaswa kutoa kiasi cha fedha kuanzia Sh50 milioni.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Singida, umeliambia Mwanaspoti mchezaji huyo amefanya mazungumzo ya awali na mabosi wa kikosi hicho tangu kwenye michuano ya Kombe la Muungano 2026, baada ya benchi la ufundi kuridhishwa na kiwango chake.
“Mazungumzo tulianza tangu michuano ya Kombe la Muungano 2026, lakini hatujafikia hitimisho na klabu inayommiliki, bado tunaendelea na suala hilo kwa sababu ni pendekezo la benchi letu la ufundi lililovutiwa naye,” kilisema chanzo hicho.
Akizungumza na Soka la Bongo, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Mlandege FC, Fatawi Ramadhan Fatawi, alisema ni kweli mazungumzo hayo kwa ajili ya mchezaji huyo na Singida yapo, japo bado mchakato unaendelea na haujafikia mwishoni.
“Ni kweli Singida inamuhitaji Mbappe na imeonyesha nia hiyo, lakini sio wao pekee kwa sababu hata Coastal Union na KMC ni miongoni mwao pia, mchezaji wetu anauzwa kuanzia Sh50 milioni na kuendelea, sio chini ya hapo,” alisema Fatawi.
Fatawi alisema uongozi wa Mlandege hauna nia ya kumzuia mchezaji anayehitajika na timu nyingine, kwa sababu wanaamini ni sehemu ya kukuza karia yake na kupata uzoefu utakaokuwa ni chachu ya kumkuza na kumfungulia fursa ya kuonekana zaidi.
Mbappe alifuatiliwa na Singida tangu alipoifunga timu hiyo bao moja kwenye ushindi wa Mlandege wa mabao 2-1, katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Muungano 2026 iliyopigwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Aprili 23, 2026.
Nyota huyo anashika nafasi ya sita katika Ligi ya Zanzibar kwa kufunga mabao mengi na hadi sasa ana 10, akizidiwa na kinara, Michael Joseph Godlove wa KVZ mwenye 16, akifuatiwa na Muslim Simai Ameir wa Kipanga aliyefunga 13.
Wengine waliomzidi Mbappe kwa mabao katika Ligi Kuu ya Zanzibar msimu huu wa 2025-2026 ni Tariq Mohamed Mkonga wa JKU na James Mlange wa Fufuni ambao kila mmoja ameshafunga 12, huku Faki Mwalimu wa Chipukizi United akifunga 11.