USHIRIKIANO WA BARKER NA UONGOZI WATAJWA KUIJENGA SIMBA YA SASA
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba SC, Crescentius Magori, amesema mafanikio ya kikosi cha sasa yanatokana na ushirikiano mzuri uliokuwepo kati ya benchi la ufundi chini ya Kocha Steve Barker na uongozi wa klabu katika mchakato wa usajili uliofanyika dirisha dogo la Januari 2026.
Magori amesema usajili wa wachezaji wapya ulifanyika kwa mashauriano ya karibu na Barker, ambaye alikuwa na ufahamu wa baadhi ya wachezaji waliolengwa.
Aidha, uongozi wa klabu ulifanya kazi ya utafutaji wa vipaji (scouting) na kumkabidhi kocha majina ya wachezaji mbalimbali kwa ajili ya tathmini kabla ya kufanyika kwa usajili.
“Kocha Barker alikuwa anawafahamu baadhi ya wachezaji tuliowalenga, huku wengine tukiwapata kupitia kazi ya uskauti. Tulishirikiana kwa karibu katika kuwafuatilia na hatimaye kufanikiwa kujenga Simba bora tunayoiona leo,” amesema Magori.
Ameeleza kuwa Simba haikuwa na bajeti kubwa ya kufanya usajili mkubwa katika dirisha hilo, jambo lililoifanya klabu kutafuta mbinu mbadala za kuimarisha kikosi bila kuathiri mipango yake ya kifedha.
Kwa mujibu wa Magori, uongozi ulifanya tathmini ya kina na kuamua kutumia fedha zilizopatikana kutokana na mauzo ya baadhi ya wachezaji wa timu hiyo ili kufanikisha usajili wa nyota wapya waliokuwa wanahitajika na benchi la ufundi.
Amesema Simba ilifanya maamuzi magumu ya kuwaachia wachezaji watatu muhimu, Jean Charles Ahoua, Steven Mukwala na Kibu Denis. Ahoua alijiunga na CR Belouizdad ya Algeria, huku Mukwala na Kibu wakihamia Al Nasri ya Libya katika dirisha la Januari.
Fedha zilizopatikana kupitia mauzo hayo ziliiwezesha Simba kusajili wachezaji wanane wapya, ambao ni kipa Djibrila Kassali, mabeki Nickson Kibabage na Ismaila Toure, viungo Libasse Gueye, Anicet Oura, Inno Loemba na Clatous Chama, pamoja na mshambuliaji Baraka Mwangosi.
Magori amesema licha ya changamoto za kifedha zilizokuwepo, Simba imefanikiwa kujenga kikosi imara chenye ushindani mkubwa. Amebainisha kuwa lengo la klabu hiyo ni kuendelea kubaki katika kiwango cha juu na kupambana kwa mafanikio katika mashindano yote inayoshiriki msimu huu.