SIMBA WAFUNGUKA KUSAKA STRAIKA MPYA WA KUONGEZA MAKALI YA USHAMBULIAJI
UONGOZI wa Simba SC umeweka wazi kuwa unaendelea na mchakato wa kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu ujao wa mashindano, huku safu ya ushambuliaji ikitajwa kuwa moja ya maeneo yanayopewa kipaumbele katika dirisha la usajili.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Crescentius Magori, amesema klabu hiyo inaendelea kufanya tathmini ya kikosi na kutafuta mchezaji wa mbele mwenye uwezo wa kuongeza ushindani na ufanisi zaidi katika eneo la ushambuliaji.
Magori alieleza kuwa pamoja na washambuliaji waliopo kufanya kazi nzuri na kutoa mchango mkubwa kwa timu, bado uongozi unaamini kuna nafasi ya kuongeza ubora zaidi ili kuifanya Simba kuwa na nguvu kubwa katika mashindano ya ndani na yale ya kimataifa.
“Kuna maeneo mawili au matatu bado tunafanyia kazi. Tunatafuta straika na tunaamini tutampata mchezaji bora zaidi ambaye ataongeza nguvu kwenye kikosi chetu.
Hili ni eneo ambalo limefanya vizuri, lakini tunaamini linaweza kufanya vizuri zaidi kama tutapata mchezaji mwenye ubora wa ziada,” amesema Magori.
Kauli hiyo imeongeza hamasa kwa mashabiki wa Simba ambao kwa sasa wanafuatilia kwa karibu harakati za usajili za klabu yao.
Wengi wao wanasubiri kuona ni nyota gani atakayetua Msimbazi kwa lengo la kuongeza makali ya mabao na kuisaidia timu kufikia malengo makubwa zaidi katika msimu ujao.