TETESI ZA MAYELE ZATIKISWA, KAMWE AFUNGUKA KILICHO NYUMA YA PAZIA
MSEMAJI wa Yanga, Ali Kamwe, ametoa kauli kuhusu mipango ya usajili wa msimu ujao huku kukiwa na tetesi zinazomhusisha aliyekuwa mshambuliaji wa klabu hiyo, Fiston Mayele, na uwezekano wa kurejea ndani ya kikosi cha Wananchi.
Mayele, ambaye amekuwa akiichezea Pyramids FC ya Misri, anaripotiwa kuwa mkataba wake na klabu hiyo umefikia tamati. Kumekuwa pia na taarifa zinazodai kuwa huenda akaendelea na soka lake katika moja ya klabu za nchi za Kiarabu.
Akizungumzia suala hilo, Kamwe alisema Mayele hatarajii kwenda kucheza katika nchi za Kiarabu, ingawa hakutaja moja kwa moja klabu au nchi ambayo nyota huyo anaelekea.
“Mayele haendi kucheza Arabuni, kuna mahali ataenda,” amesema Kamwe.
Mbali na kauli hiyo kuhusu Mayele, Kamwe amesisitiza kuwa Yanga inaendelea na maandalizi makubwa ya kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu ujao, akieleza kuwa mashabiki wanapaswa kutarajia timu yenye ushindani mkubwa kutokana na mikakati ya usajili inayoendelea.
Amebainisha kuwa viongozi wa klabu wamefanya kazi kubwa katika kusajili na kukamilisha taratibu za kuwapata baadhi ya wachezaji watakaoongeza nguvu ndani ya kikosi hicho.
“Kwa msimu ujao, naomba Bodi ya Ligi mechi yetu ya kwanza watupange na Dodoma Jiji FC. Tutakuwa moto kutokana na mikakati yetu ya usajili na namna tunavyoendelea kuimarisha kikosi chetu,” amesema Kamwe.
Kauli hiyo imezidi kuongeza hamasa kwa mashabiki wa Yanga ambao kwa sasa wanafuatilia kwa karibu hatua za usajili za klabu hiyo kuelekea msimu mpya wa mashindano.