MWEZI MGUMU KWA YANGA, LIGI NA KOMBE VYATOA MTIHANI MKUBWA
KIKOSI cha Yanga kinatarajiwa kurejea kambini rasmi Jumatatu, Juni 1, 2026, kwa ajili ya kujiandaa na michezo ya mwisho ya Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Kombe la Shirikisho la CRDB.
Msemaji wa klabu hiyo, Ali Kamwe, amesema safari ya kusaka alama 15 katika mechi tano zilizobaki haitakuwa nyepesi kutokana na ushindani mkubwa uliopo katika hatua hii ya mwisho ya msimu.
Baada ya ligi kurejea Juni 10, Yanga itaanza kampeni yake kwa safari ngumu ya kwenda Kigoma kuikabili Mashujaa FC kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mechi ambayo Kamwe amesema inahitaji maandalizi ya hali ya juu ili kuhakikisha timu inapata matokeo chanya.
Kamwe amesema klabu imeanza kuwaandaa wachezaji na mashabiki wake kuelekea michezo hiyo mitano iliyosalia, huku akisisitiza kuwa hakuna mchezo mwepesi katika harakati za kutetea ubingwa wa ligi. Yanga itakutana na Mashujaa FC, Fountain Gate FC, Azam FC, TRA United na JKT Tanzania katika mechi zake zilizobaki.
“Mechi tano zilizobaki zote ni ngumu, hakuna mpinzani mwepesi hapo. Mashujaa FC, Fountain Gate FC, Azam FC, TRA United na JKT Tanzania zote ni mechi dume ambazo zinahitaji umakini mkubwa,” amesema Kamwe.
Ametolea mfano mchezo uliopita dhidi ya Dodoma Jiji, akisema wengi hawakutarajia ungekuwa mgumu kwa Yanga, lakini matokeo yalionyesha kuwa kila timu ina uwezo wa kusababisha mshangao. Kutokana na hilo, amewataka wachezaji na mashabiki kutowadharau wapinzani waliobaki.
“Hizi mechi za mwisho lazima tujiandae vizuri na tusiende kichwa kichwa. Ukamchukulia poa mpinzani, anaweza kukushangaza wakati wowote,” ameongeza.
Kwa upande wa maandalizi, Kamwe amesema wachezaji waliopo nchini wataanza mazoezi Juni 1, huku wale walioko kwenye majukumu ya timu za taifa wakitakiwa kurejea salama bila majeraha ili kuimarisha kikosi kuelekea ratiba hiyo muhimu ya mwisho wa msimu.
Mbali na mechi tano za ligi, Yanga pia inatarajiwa kucheza michezo miwili ya Kombe la Shirikisho la CRDB, jambo linaloufanya mwezi Juni kuwa na ratiba ngumu kwa mabingwa hao watetezi.
“Tunatakiwa kutetea mataji yetu. Ni muhimu tuwekeze nguvu zetu zote kuhakikisha tunafanikiwa kushinda kila taji lililo mbele yetu msimu huu,” amesema Kamwe.