MPANGO WA SIRI WA SIMBA WAMHUSISHA BEKI WA MAMELODI SUNDOWNS
KLABU ya Simba imeanza mipango ya kuimarisha safu yake ya ulinzi kuelekea msimu ujao, huku Kocha Mkuu Steve Barker akitajwa kuvutiwa na huduma za beki wa kushoto wa Mamelodi Sundowns, Fawaaz Basadien.
Taarifa kutoka ndani ya klabu zinaeleza kuwa Barker anataka kufanya kazi tena na mchezaji huyo aliyewahi kumfundisha akiwa Stellenbosch FC.
Kocha huyo anaamini Basadien ana uwezo wa kuongeza ubora, ushindani na uthabiti katika eneo la ulinzi la Wekundu wa Msimbazi.
Chanzo hicho kimebainisha kuwa Simba inaangalia uwezekano wa kumsajili Basadien kwa mkopo wa msimu mmoja, huku Barker akiwa mstari wa mbele kushawishi viongozi wa klabu kuanza mazungumzo na Mamelodi Sundowns.
“Barker anataka kuungana tena na mchezaji wake wa zamani, Fawaaz Basadien. Kuna uwezekano mkubwa wa kujiunga na Simba kwa mkopo.
Kocha huyo amewashawishi viongozi wa klabu kuwasiliana na Sundowns ili kuona uwezekano wa kumpata kwa muda na kumpa nafasi zaidi ya kucheza,” kilisema chanzo hicho.
Kwa sasa, Basadien anakabiliwa na ushindani mkubwa ndani ya kikosi cha Sundowns kutokana na uwepo wa nyota kama Divine Lunga, Aubrey Modiba na Khuluman Ndamane, hali ambayo imepunguza muda wake wa kucheza mara kwa mara.
Kutokana na mazingira hayo, inaelezwa kuwa mlinzi huyo anaweza kuvutiwa na wazo la kutafuta changamoto mpya kwa muda ili kupata dakika nyingi zaidi uwanjani na kurejesha kiwango chake cha juu.
Barker anamfahamu vyema Basadien tangu walipokuwa pamoja Stellenbosch FC, ambako beki huyo alikuwa miongoni mwa wachezaji muhimu wa kikosi hicho. Uhusiano wao wa muda mrefu unatajwa kumpa kocha huyo imani kuwa mchezaji huyo ataweza kuendana haraka na mfumo wa Simba.
Mbali na kucheza nafasi ya beki wa kushoto, Basadien pia ana uwezo wa kucheza katika mfumo wa mabeki watatu akiwa upande wa kushoto wa safu ya ulinzi. Uwezo huo wa kucheza nafasi zaidi ya moja unamfanya kuwa chaguo linalovutia kwa falsafa ya soka ya Barker.
Iwapo dili hilo litafanikiwa, Simba itakuwa imeongeza mchezaji mwenye uzoefu mkubwa na anayefahamu mahitaji ya kocha wake. Aidha, Basadien anaweza kuungana tena na Neo Maema, jambo linaloweza kuongeza ushindani na uimara katika safu ya ulinzi ya Wekundu wa Msimbazi.