Simba SC

SIMBA SC YAANZA OPERESHENI ALAMA 15, YAREJEA KAMBINI KWA VITA YA UBINGWA

Vardo May 31, 2026 12:20 pm

BAADA ya mapumziko mafupi, kikosi cha Simba SC kinatarajiwa kurejea kambini kesho (Jumatatu) kuanza maandalizi ya mwisho kuelekea michezo mitano iliyobaki ya Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa na lengo la kuvuna alama zote 15 ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutimiza malengo yake ya msimu.

 

Kwa mujibu wa ratiba iliyopo, Simba itacheza mechi tatu za nyumbani dhidi ya Pamba Jiji FC, Singida Black Stars na KMC FC, huku ikitarajiwa kucheza mechi mbili za ugenini dhidi ya Mbeya City na Mtibwa Sugar.

 

Safari ya Simba itaanza kwa mchezo dhidi ya Pamba Jiji FC utakaochezwa katika Uwanja wa KMC Complex, Mwenge. Baada ya hapo, wekundu hao wa Msimbazi watasafiri kwenda Mbeya kuvaana na Mbeya City kabla ya kuelekea Morogoro kukabiliana na Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Jamhuri.

Baada ya kumaliza mechi hizo za ugenini, Simba itarejea nyumbani kwa michezo miwili ya mwisho dhidi ya Singida Black Stars na KMC FC, ambayo nayo inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa huku kila timu ikisaka kutimiza malengo yake.

Akizungumzia maandalizi hayo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema kikosi hicho kinaingia kambini kikiwa na morali kubwa na dhamira ya kuhakikisha kinapata ushindi katika kila mchezo uliosalia bila kujali ukubwa wa mpinzani.

“Baada ya mapumziko mafupi, kesho (Jumatatu) tunaingia kambini kujiandaa na michezo mitano iliyosalia ya ligi pamoja na michezo miwili ya Kombe la Shirikisho la CRDB ambayo ni nusu fainali na fainali.

Tuna kikosi bora kinachotupa jeuri na kujiamini kwamba tunaweza kufanya vizuri kwa sababu tunahitaji kutwaa mataji yote mawili,” amesema Ahmed.

Ahmed ameongeza kuwa ana imani wachezaji wote ambao kwa sasa wako katika majukumu ya timu za taifa watarejea salama na kuungana na wenzao kambini ili kuendeleza kasi waliyoionyesha kabla ya mapumziko.

Kwa sasa, Simba inaelekeza nguvu zake katika kuhakikisha inamaliza msimu kwa mafanikio makubwa, huku ikisaka kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho la CRDB.

NJIA YA KNICKS KUREJEA FAINALI BAADA YA MIAKA 27 MBINGWA YANGA WAANZA MAPEMA USAJILI MKUBWA WA MSIMU UJAO