NJIA YA KNICKS KUREJEA FAINALI BAADA YA MIAKA 27
NEW YORK, MAREKANI: BAADA ya kusubiri kwa miaka 27, hatimaye New York Knicks imerejea katika ngazi kubwa zaidi ya mpira wa kikapu duniani, Fainali za NBA.
Ni mafanikio ambayo miaka michache iliyopita yalionekana kama ndoto kwa mashabiki wa timu hiyo maarufu ya Jiji la New York lakini leo hii, Knicks imebaki hatua nne tu kutoka kutwaa ubingwa wake wa kwanza katika enzi ya familia ya Dolan.
Knicks imekata tiketi ya kucheza Fainali za NBA 2026 baada ya kuibuka bingwa wa Ukanda wa Mashariki (Eastern Conference) kwa kuifagia Cleveland Cavaliers kwa ushindi wa 4-0. Knicks ilihakikisha nafasi hiyo baada ya ushindi mkubwa wa pointi 130-93 katika Game 4 na hivyo kurejea Fainali za NBA kwa mara ya kwanza baada ya miaka 27 tangu ilipocheza hatua hiyo mwaka 1999. Mafanikio hayo yametajwa kujengwa kwa mipango makini, usajili wa maana, mabadiliko ya kimkakati na maamuzi magumu yaliyofanywa na rais wa mpira wa kikapu wa timu hiyo, Leon Rose.
Wakati James Dolan alipokuwa akitafuta mtu wa kuiongoza Knicks katika mafanikio, wengi walidhani angechagua mchezaji wa zamani au mtendaji mwenye uzoefu mkubwa wa kuendesha timu za NBA.
Badala yake, Dolan alimchagua Rose, aliyekuwa wakala maarufu wa wachezaji wakubwa akiwemo LeBron James na Allen Iverson.
Wengi waliona uamuzi huo kuwa hatari kwa sababu Rose hakuwa na uzoefu wa kuendesha ofisi ya timu ya NBA. Lakini miaka sita baadaye, uamuzi huo unaonekana kuwa moja ya maamuzi bora kabisa katika historia ya Knicks.
Tangu alipowasili mwaka 2020, Rose ameunda kikosi kilichojaa vipaji tofauti. Hakutegemea Draft pekee, bali alitumia usajili wa wachezaji huru, biashara za kubadilishana wachezaji na hata fursa zilizojitokeza ghafla sokoni. Nyota mkubwa wa mradi huo ni Jalen Brunson. Mchezaji huyo alisajiliwa kama mchezaji huru mwaka 2022 akitokea Dallas Mavericks. Wakati huo wengi walimuona kama mlinzi wa kawaida, lakini Knicks amegeuka kuwa mmoja wa walinzi bora zaidi NBA.
Brunson amekuwa moyo wa timu hiyo, kiongozi wa chumba cha kubadilishia nguo na silaha kuu ya ushambuliaji. Uwezo wake wa kufunga, kutengeneza nafasi na kuhimili presha umekuwa msingi wa mafanikio ya Knicks msimu huu.
Baada ya kupata kiongozi wao, Knicks walifanya biashara kubwa mwaka 2024 kwa kumchukua Karl-Anthony Towns kutoka Minnesota Timberwolves.
Ilikuwa biashara iliyomtoa Julius Randle, lakini viongozi wa Knicks waliamini Towns angeendana vizuri zaidi na mfumo wa Brunson.
Tangu ajiunge na timu hiyo, Towns ameongeza nguvu, uwezo wa kufunga kutoka maeneo mbalimbali pamoja na pasi zake ambazo zimekuwa silaha muhimu katika hatua za mtoano.
Katika safu ya ulinzi, Knicks ilifanya kazi kubwa kwa kumleta OG Anunoby kutoka Toronto Raptors. Anunoby amekuwa mchezaji muhimu sana katika kuzuia nyota wa timu pinzani. Uwezo wake wa kulinda nafasi nyingi na kuchangia pointi umeifanya Knicks kuwa moja ya timu ngumu zaidi kuchezewa katika NBA.
Mwaka uliofuata, Knicks ilifanya tena biashara kubwa kwa kumchukua Mikal Bridges kutoka Brooklyn Nets. Wakati huo mashabiki wengi walihoji uamuzi wa kutoa chaguo tano za raundi ya kwanza ya Draft ili kumpata Bridges. Mwanzo wake haukuwa mzuri, lakini kadri msimu ulivyoendelea alianza kurejesha kiwango chake na sasa amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu katika safari ya Knicks kuelekea Fainali.
Miongoni mwa mastaa ambao hawapati sifa nyingi lakini wamekuwa muhimu sana ni Josh Hart. Mchezaji huyo amekuwa mfano wa kujituma, kupambana na kucheza kwa moyo. Ingawa si mfungaji mkubwa, mchango wake katika reboundi, ulinzi na kuhamasisha wenzake umeifanya Knicks kuwa timu yenye ushindani mkubwa.
Mitchell Robinson ndiye mchezaji aliyekaa muda mrefu zaidi ndani ya kikosi hicho. Akiwa amechaguliwa katika Draft ya mwaka 2018, amebaki kuwa nguzo muhimu katika kulinzi. Katika benchi la ufundi, Knicks ilifanya uamuzi mwingine mkubwa kwa kumteua Mike Brown kuwa kocha mkuu mwaka 2025.
Brown alikuwa amefukuzwa kazi mara kadhaa katika timu tofauti za NBA jambo lililofanya baadhi ya watu kuhoji uteuzi wake. Lakini ndani ya muda mfupi ameonyesha uwezo mkubwa wa kuiongoza timu hiyo. Mbinu zake za kiufundi, uwezo wa kuwasimamia wachezaji wakubwa na uzoefu wake wa kufanya kazi pamoja na Steve Kerr huko Golden State Warriors vimemsaidia kuibadilisha Knicks.
Mbali na nyota wakubwa, Knicks imefaidika pia na mchango wa Landry Shamet, Jordan Clarkson, Jose Alvarado na Miles McBride ambao wamekuwa wakitoa msaada mkubwa wanapoingia kutoka benchi.
Mchanganyiko huo wa mastaa, wachezaji wa kazi maalumu na viongozi makini umeifanya Knicks kuwa moja ya timu bora zaidi katika NBA msimu huu.
Kwa sasa Jiji la New York linaota ndoto ya kuona timu yake ikinyanyua ubingwa wa NBA baada ya miaka 27 ya kusubiri, Knicks imerudi kwenye fainali. Safari imekuwa ndefu, yenye maumivu na changamoto nyingi, lakini sasa wako hatua nne tu kutoka kuandika historia mpya.