Habari za michezo

MASHABIKI WA ARSENAL, PSG WAZICHAPA

Vardo May 31, 2026 10:16 am

BUDAPEST, HUNGARY: MASHABIKI wa Arsenal wamepigana na wenzao wa PSG katika mitaa ya Budapest, Hungary, kabla ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyopigwa jana usiku kwenye Uwanja wa Uwanja wa Puskas Arena, matukio ambayo yalidaiwa kuwa kipimo kwa polisi wa nchi hiyo kukabiliana na vurugu za wapenzi wa soka.

Hungary ina timu mbili kubwa ambazo ni Ferencvarosi TC and Ujpest ambazo hata hivyo hazina mashabiki wanazi kama zilivyo timu za Ulaya Magharibi zinazokotokea Arsenal na PSG, ambazo mashabiki wake walianza kutambiana mapema mitaani, huku walitoka London wengi wao wakigeuza katikati ya Jiji la Budapest kuwa kama kwao.

Video zilizosambaa mitandaoni zilionyesha mapigano yakizuka kati ya makundi ya mashabiki kwenye Mtaa wa Kiraly wakipigana kwa mateke na ngumi, huku wengine wakirusha fataki na kuligeuza eneo hilo kuwa jekundu kabla ya kukabiliwa na polisi waliofanikiwa kuwatawanya kwa mabomu ya machozi.

Vurugu ndogo kati ya mashabiki wa timu hizo zilianza tangu juzi usiku video zikionyesha makundi kadhaa yakirushiana maneno mitaani.

Katika tukio jingine, saa 10 jioni kwa saa za Budapest , jana Jumamosi, raia mmoja wa Uingereza alikamatwa baada ya kuhusika katika ugomvi na raia wawili wa Ureno kwenye moja ya milango ya eneo maarufu la Champions Festival. Wote watatu walikamatwa na kushtakiwa kwa kufanya vurugu. Raia mwingine wa Uingereza alikamatwa saa 5 usiku baada ya kupanda juu ya gari na kuliharibu.

Nao mashabiki wa PSG walisikika wakipiga kelele na kuomba msaada kutoka kwa maofisa wa polisi katika mtaa mwingine uliopo jirani na eneo hilo, suala ambalo baadaye msemaji wa polisi alisema walikuwa wanalifanyia uchunguzi kuwatambua waliohusika ili hatua zichukuliwe.

Na katika mtaa mwingine mashabiki wawili wa Arsenal walikamatwa kwa tuhuma za kufanya vurugu na kuharibu gari. Matukio hayo yote yaliripotiwa kabla ya maofisa 4,000 polisi hawajatawanywa mitaani kwa ajili ya kuhakikisha usalama usiku ikiaminika kwamba takriban mashabiki 10,000 wangewasili bila tiketi za mechi hiyo ili kulazimisha kuingia uwanjani au kusambaa mitaani kujiandaa kusherehekea ubingwa.

Katika mkutano na waandishi wa habari, Meja Jenerali Dk Janos Zoltan Kuczik, kamanda wa operesheni za fainali hiyo, alionya kwamba  watachukua hatua kali ikiwa watakutana na tabia yoyote inayovuruga utulivu wa umma.

“Sio siri kwamba kuwa na mashabiki kutoka London na Paris mjini Budapest kwa wakati mmoja kunaleta hatari kubwa, lakini ni jukumu letu kupunguza hatari hiyo,” alisema

KUTOKA UBINGWA WA PELE HADI HEADBUTT YA ZIDANE NJIA YA KNICKS KUREJEA FAINALI BAADA YA MIAKA 27