KUTOKA UBINGWA WA PELE HADI HEADBUTT YA ZIDANE
MIAMI, MAREKANI: WAKATI fainali za Kombe la Dunia 2026 zikibakiza takriban wiki tatu na ushee, mambo ni moto! Tayari timu za mataifa mbalimbali zinazopigana vikumbo kukiwasha mwaka huu huko Marekani, Canada na Mexico zimeanza kupanga majeshi na zipo zilizotangaza vikosi vya awali vya nyota 55 wakitarajiwa kupungua hadi kati ya 23 na 26.
Hilo limekuwa hivyo ili kutoa fursa kwa makocha wa nchi 48 zinazotarajiwa kushiriki fainali hizo kupewa muda wa kufanya tathmini kabla ya kutangaza vikosi kamili wiki mbili kabla ya kuanza kwa michuano hiyo inayoanza Juni 11 hadi Julai 19, mwaka huu.
SA ITAKUWAJE?
Baada ya kutwaa taji lake la kihistoria Qatar miaka minne iliyopita, Lionel Messi na kikosi cha Argentina wanaenda kwenye Kombe la Dunia wakiwa katika harakati za kuhitimisha safari nyota huyo kwa hadithi ya kusisimua.
Mchezaji huyo maarufu wa soka alijiweka kwenye historia aliponyanyua Kombe la Dunia 2022, jambo lililowafanya wengi kuamini mjadala wa nani ni “GOAT” (mchezaji bora wa muda wote) ulikuwa umefungwa baada ya kuiongoza Argentina kwenye ushindi.
Kombe la Dunia lilikuwa ndilo taji pekee lililokuwa halipo kwenye mkusanyiko wa mafanikio ya Messi, baada ya kukaribia kulitwaa 2014 aliposhindwa fainali. Wengi waliamini michuano ya 2022 ilikuwa nafasi yake ya mwisho ya kutwaa ubingwa huo na gwiji huyo wa zamani wa Barcelona hakupoteza nafasi hiyo kwani alifunga mabao saba na kuwa nyota katika ushindi wa kwanza wa Argentina tangu 1986.
Sasa, miaka minne baadaye, Messi na Argentina wanaenda Marekani, Canada na Mexico wakitaka kujiweka miongoni mwa timu bora zaidi kuwahi kutokea katika soka la kimataifa. Argentina inaweza kuwa taifa la tatu pekee kutwaa ubingwa huo mara mbili mfululizo katika kile kinachoonekana Kombe la Dunia la mwisho kwa Messi mwenye umri wa miaka 38.
Lakini mwisho wake wa safari ya Kombe la Dunia utafananishwaje na mastaa wengine wakubwa waliomtangulia? talkSPORT imeangalia historia.
CR7 Bado haijaisha
Kutoka Ronaldo mmoja hadi mwingine! Kabla ya Kombe la Dunia la Qatar 2022, mashabiki wengi waliamini mashindano hayo yangetoa jibu la mwisho kuhusu nani ni GOAT kati ya Cristiano Ronaldo na Messi, katika kile kilichoonekana kuwa mashindano yao ya mwisho ya Kombe la Dunia.
Na ingawa sasa inatarajiwa kuonwa “ngoma ya mwisho” kutoka kwa mastaa hao wawili wa karne ya 21, wengi hawatasahau machozi ya Ronaldo alipoyaaga mashindano hayo miaka minne iliyopita.
Akiwa na umri wa miaka 37 wakati huo, nahodha huyo wa Ureno alionekana kumpiku Messi alipokuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao katika Kombe la Dunia tano tofauti baada ya kufunga dhidi ya Ghana kwenye mchezo wa ufunguzi.
Hata hivyo, alipoteza nafasi yake kwenye kikosi cha kwanza kufuatia madai ya kutofautiana na kocha Fernando Santos. Na Ronaldo alitokwa na machozi baada ya kushindwa kuizuia Ureno kutolewa kwa kufungwa bao 1-0 na Morocco.
Matokeo hayo yalimaanisha kuwa nyota huyo wa zamani wa Manchester United alimaliza michezo yote minane ya hatua ya mtoano ya Kombe la Dunia bila kufunga bao lolote, licha ya kupiga mashuti 27 ndani ya dakika 570.
Ronaldo Nazario hadithi ya kufikirika
Ronaldo Nazario “El Fenomeno” ataendelea kukumbukwa kama mmoja wa washambuliaji bora kuwahi kucheza soka na sehemu kubwa ya urithi huo ilitokana na maajabu yake katika Kombe la Dunia 2002.
Ronaldo alikuwa na miaka 17 alipochaguliwa kwenye kikosi cha Brazil cha Kombe la Dunia 1994, lakini hakupata nafasi ya kucheza huku Brazil ikitwaa ubingwa. Miaka minne baadaye, mshambuliaji huyo wa zamani wa Barcelona alikuwa mchezaji bora zaidi duniani alipoipeleka Brazil hadi fainali ya pili mfululizo, lakini tatizo la kiafya alilopata kabla ya mchezo huo lilisababisha Ufaransa kushinda 3-0.
Mchezaji huyo alitumia miaka iliyofuata akisumbuliwa na majeraha, lakini alirejea kwa nguvu 2002 na kuandika upya historia yake ya Kombe la Dunia. Na kweli alifanya kile kilichotarajiwa na dunia ya soka akifunga mabao mawili kwenye fainali dhidi ya Ujerumani huku akitwaa Kiatu cha Dhahabu na kuisaidia Brazil kushinda Kombe la Dunia la tano.
Kombe lake la mwisho 2006 lilikuja wakati akiwa amepungua kiwango, lakini bado alifunga mabao matatu yaliyomfanya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa mashindano hayo kwa mabao 15, rekodi iliyodumu kwa miaka minane hadi ilipovunjwa na Miroslav Klose 2014.
Pele na hadithi ya kifalme
Katika kiwango chake bora, Pele aliichezea Santos, lakini kila baada ya miaka minne alitumia Kombe la Dunia kuuonyesha ulimwengu uwezo wake. Nyota huyo ambaye jina lake kamili ni Edson Arantes do Nascimento alijitangaza 1958 akiwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kushinda Kombe la Dunia akiwa na miaka 17, akifunga mabao sita, mawili kati yake kwenye ushindi wa 5-2 dhidi ya Sweden katika fainali.
Pele alikuwa sehemu ya kikosi cha Brazil kilichotetea taji miaka minne baadaye, lakini alipata majeraha mapema kwenye mashindano.
Katika Kombe la Dunia 1966, Pele alifanyiwa faulo nyingi kiasi kwamba alitangaza kuwa hiyo ilikuwa fainali yake ya mwisho ya Kombe la Dunia, lakini baadaye alibadilisha uamuzi huo kabla ya Mexico 1970. Na gwiji huyo alihakikisha anamaliza safari yake kwa mtindo wa kipekee aliposhinda Kombe la Dunia la tatu.
Katika mechi yake ya mwisho ya Kombe la Dunia, Pele aliiongoza Brazil kuifunga Italia 4-1 huku akifunga bao moja na kusaidia mawili.
Zinedine Zidane na mwisho wa kusikitisha
Neno “headbutt” kwa Kiswahili linaweza kutafsiriwa kama kumpiga mtu kwa kichwa au kumtandika kichwa na mfano kwenye medani za michezo ni kama ambavyo Zinedine Zidane alivyompiga kichwa Marco Materazzi wa Italia kwenye fainali ya Kombe la Dunia 2006.
Fainali hiyo ilitakiwa kuwa mwisho mzuri wa mmoja wa wachezaji bora kabisa kuwahi kucheza soka, lakini badala yake ikawa kumbukumbu mbaya. Zidane maarufu Zizou alikuwa nyota wa ushindi wa kwanza wa Ufaransa wa Kombe la Dunia nyumbani 1998.
Nyota huyo wa zamani wa Real Madrid alipata kadi nyekundu kwa kumkanyaga mchezaji wa Saudi Arabia kwenye hatua ya makundi, lakini alirejea na kuiongoza Ufaransa kutwaa ubingwa kwa kuifunga Brazil mabao 3-0 kwenye fainali huku akifunga mabao mawili.
Jeraha la paja lilimzuia Zidane kucheza kwa kiwango chake 2002 huku Ufaransa ikitolewa mapema kwa kumaliza mkiani mwa kundi. Zizou alikuwa akitarajia kumaliza kazi yake kwa ubora 2006 wakati Ufaransa iliporejea tena fainali. Alifunga bao la kuongoza dhidi ya Italia kabla ya kutolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumpiga kichwa Materazzi, na akalimwa kadi nyekundu huku timu yake ikipoteza kwa penalti.
Franz Beckenbauer na hadithi ya kifalme
Franz Beckenbauer maarufu Der Kaiser ana hoja kubwa ya kuitwa staa bora zaidi kuwahi kutokea kwenye fainali za Kombe la Dunia akiwa mmoja wa watu watatu pekee waliowahi kushinda taji hilo kama mchezaji na kocha. Kombe lake la kwanza 1966 lilimshuhudia akimaliza akiwa mfungaji wa tatu bora huku Ujerumani Magharibi ikifungwa na England kwenye fainali.
Miaka minne baadaye, Beckenbauer alicheza akiwa na mkono kwenye ‘kombeo’ baada ya kuteguka bega kwenye nusu fainali na ushindi wa Italia wa mabao 4-3 kwenye mchezo huo baadaye ulipewa jina la “Mchezo wa Karne”. Mwaka 1974 akiwa nahodha na akicheza beki, aliisaidia Ujerumani Magharibi kuizuia Uholanzi ya Johan Cruyff na kushinda Kombe la Dunia nyumbani.
Na miaka 16 baadaye, alinyanyua tena kombe hilo kama kocha wa Ujerumani Magharibi baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Argentina katika mechi yake ya mwisho akiwa kocha wa timu hiyo.
Diego Maradona na mwisho wa fedheha
Messi amebeba mzigo wa kujaribu kufikia mafanikio ya Maradona kwenye Kombe la Dunia katika maisha yake ya soka la kimataifa, lakini kwa mshangao mechi yake ya mwisho kwenye mashindano hayo inaweza kuwa ya furaha kubwa ambayo Maradona hakuwahi kuipata.
Mwaka 1986, Maradona alikuwa nahodha aliyeibeba Argentina hadi ubingwa, akifunga bao linalotajwa kuwa bora zaidi kwenye historia ya Kombe la Dunia pamoja na lile lililoleta mabishano makubwa dhidi ya England.
Miaka minne baadaye alikuwa amepungua kiwango, lakini bado alikaribia kuisaidia Argentina kutetea ubingwa. Katika Kombe la Dunia huko Marekani 1994, Maradona alikusudia kuaga mashindano hayo kwa ‘uchawi wa mwisho’ kwa bao kali kwenye ushindi wa 4-0 dhidi ya Ugiriki. Lakini alifukuzwa kwenye mashindano hayo kwa fedheha baada ya kupimwa na kukutwa na dawa ya kuongeza nguvu.