Michezo Bongo

WPL KUNA MOTO UNAWAKA

Vardo May 31, 2026 10:08 am

LIGI Kuu ya Wanawake (WPL) inaendelea Mei 31, 2026 kwa mechi sita, lakini macho ya wengi yataelekezwa Uwanja wa KMC Complex na vinara Simba Queens watakuwa na kibarua dhidi ya Mashujaa Queens katika pambano linaloweza kuamua ubingwa.

Simba inaongoza msimamo kwa pointi 53 baada ya kucheza mechi 19, ikifuatiwa na Yanga Princess yenye pointi 43, huku JKT Queens ikiwa na pointi 42 lakini ikiwa imecheza mechi 18.

Hii ni raundi ya 20 ya WPL na kwa hesabu za ubingwa, Simba Queens inahitaji hata sare tu dhidi ya Mashujaa Queens ili kutangazwa mabingwa wapya zikiwa zimesalia mechi mbili.

Hata hivyo, mechi hiyo haitakuwa rahisi kama baadhi ya watu wanavyofikiria. Mashujaa Queens imekuwa moja ya timu zinazofanya vizuri. Hivi karibuni ilionyesha upinzani dhidi ya JKT Queens na kutoka 0-0, pia ikaonyesha ushindani mkubwa dhidi ya Yanga matokeo yakiwa 0-0 kabla ya kuifunga Ceasiaa Queens mabao 2-1.

Kutokana na mwenendo huo, Mashujaa inaingia uwanjani ikiwa na imani ya kuendelea kuvuruga hesabu za vigogo. Pia inapigania kulinda nafasi ya nne ambayo imeanza kutishiwa na Fountain Gate Princess iliyoko nyuma kwa tofauti ya pointi tatu.

Wakati Simba ikisaka pointi moja ya kuunyakua ubingwa, pambano lingine kubwa litakuwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo la JKT Queens dhidi ya Yanga.

Tofauti ya timu hizo ni pointi moja tu, lakini JKT inasubiri uamuzi kama itapewa pointi tatu za mezani baada ya Ruangwa Queens kutofika kwenye mechi iliyopita, hivyo inaweza kuwa juu ya Yanga. Hilo linaifanya mechi hiyo kuwa kama fainali ya nafasi ya pili.

Yanga imekuwa ikisuasua baada ya kuangusha pointi saba katika michezo yao minne ya mwisho. Matokeo hayo yameiondoa kwenye mbio za ubingwa na sasa inapaswa kupambana kulinda nafasi ya pili.

Kwa upande wa JKT Queens ambayo ni bingwa mtetezi, ushindi utaipandisha juu ya Yanga na kuipa nafasi nzuri ya kumaliza msimu nafasi ya pili.

VITA YA NAFASI YA NNE

Mashujaa itakuwa na jicho moja kwenye mchezo dhidi ya Simba na jingine Karume ambako Fountain Gate Princess itakuwa mgeni wa Bunda Queens.

Mashujaa ina pointi 33 huku Fountain Gate ikiwa na pointi 30. Ushindi wa Fountain Gate na matokeo mabaya kwa Mashujaa unaweza kufufua kwa kiasi kikubwa mbio za kuwania nafasi ya nne.

MKIANI SIO SALAMA

Alliance Girls itakuwa nyumbani dhidi ya Ruangwa Queens katika mechi muhimu kwa timu zote mbili. Ruangwa bado inapambana kujinasua kutoka mkiani huku Alliance ikisaka kumaliza msimu katika nafasi nzuri zaidi.

Ceasiaa na Bilo Queens zitakutana Samora katika mechi ya kujinusuru na kumaliza msimu kwa heshima, wakati Geita Gold Queens itakuwa nyumbani dhidi ya Tausi FC.

Huu ukiwa ni msimu wa nane wa Ligi Kuu Soka Wanawake Tanzania Bara, Simba tayari imechukua ubingwa mara nne sawa na JKT huku Mlandizi Queens ikibeba mara moja.

MERIDIANBET YATOA TABASAMU WODINI ILI KUJENGA KESHO BORA KUTOKA UBINGWA WA PELE HADI HEADBUTT YA ZIDANE