Simba SC

SIMBA WAAHIDI MAJINA MAZITO, STRAIKA MPYA KUONGEZA NGUVU

Vardo May 31, 2026 3:42 pm

SIMBA SC imeendelea kutuma ishara za wazi kwamba haichezi mbali na maboresho makubwa kuelekea msimu ujao, baada ya uongozi wake kuweka bayana dhamira ya kuimarisha kikosi kupitia dirisha la usajili linaloendelea.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, Crescentius Magori, amesema Simba bado ipo sokoni na haijafunga milango ya kuwasaka wachezaji bora wa kigeni watakaoweza kuongeza ushindani ndani ya kikosi.

 

Magori amesisitiza kuwa malengo ya klabu si kujaza tu nafasi zilizo wazi, bali ni kuleta wachezaji wenye kiwango cha juu zaidi kuliko waliopo sasa, hatua anayoamini itainua ubora wa timu ndani na nje ya nchi.

“Kuna mambo mawili; bado tunafanyia kazi usajili wa baadhi ya wachezaji wa kigeni kwa sababu tunataka kuleta wachezaji wazuri zaidi ambao wataongeza nguvu ya kikosi chetu kuliko tulipofikia sasa,” amesema Magori.

 

Ameongeza pia kuwa eneo la ushambuliaji ndilo linaangaliwa kwa macho ya karibu zaidi, akibainisha kuwa Simba inaendelea kumtafuta straika namba 9 mwenye uwezo wa kuleta tofauti kubwa kwenye matokeo ya timu.

“Tunatafuta straika na tunaamini tutapata mchezaji bora zaidi kuliko tulionao kwa sasa. Ni kweli eneo hilo linafanya vizuri, lakini tunaamini lingeweza kufanya vizuri zaidi kama tungekuwa na wachezaji bora zaidi,” ameongeza.

Kauli hiyo imezua msisimko kwa mashabiki wa Simba SC, ambao sasa wanasubiri kuona ni majina gani mapya yatakayowasili Msimbazi, huku maandalizi ya msimu mpya yakiendelea chini ya benchi la ufundi na uongozi wa klabu hiyo.

ALIYEKUWA MWENYEKITI WA BODI YA MCL, LEONARD MUSUSA AFARIKI DUNIA ARNE SLOT AINGIA RADA ZA AC MILAN