BARKER ATAKA MBADALA WA MWALIMU, SOPU APEWA KIPAUMBELE
UONGOZI wa Simba SC umeonyesha dhamira kubwa ya kutekeleza mahitaji ya Kocha Mkuu, Steven Barker, katika dirisha la usajili kwa kutenga fedha nyingi kwa ajili ya kuwania saini ya mshambuliaji wa Azam FC, Abdul Suleiman maarufu kama Sopu.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa Simba imeongeza kasi ya maboresho ya kikosi chake kuelekea msimu ujao, huku Sopu akiwa miongoni mwa wachezaji wanaopewa kipaumbele kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufunga mabao na uzoefu wake katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Inaelezwa kuwa mabosi wa Msimbazi tayari wamewasilisha ofa yenye maslahi makubwa kwa mshambuliaji huyo, ikijumuisha mshahara mzuri, ada ya usajili pamoja na mkataba wa miaka miwili, wakiamini hatua hiyo inaweza kumshawishi kujiunga na klabu hiyo baada ya kumalizika kwa msimu wa sasa.
Sopu, ambaye hivi karibuni amerejea uwanjani baada ya kuuguza majeraha yaliyomuweka nje kwa kipindi fulani, anaripotiwa kuvutiwa na mpango wa Simba na anatarajiwa kufanya uamuzi kuhusu hatma yake baada ya kukamilisha majukumu yake na Azam FC.
Pamoja na hilo, Azam FC bado haijakata tamaa ya kumbakiza nyota huyo na inaendelea kufanya mazungumzo kwa lengo la kumuongezea mkataba na kuendelea kuwa sehemu ya kikosi chao katika misimu ijayo.
Iwapo dili hilo litakamilika, Simba itakuwa imepata nyongeza muhimu katika safu yake ya ushambuliaji, hasa baada ya mshambuliaji Seleman Mwalimu kumaliza kipindi chake cha mkopo na kutarajiwa kurejea katika klabu yake ya Wydad AC ya Morocco.
Barker anaonekana kumtazama Sopu kama chaguo bora la mshambuliaji mzawa atakayesaidia kuimarisha ushindani wa kikosi hicho katika mashindano ya ndani na kimataifa msimu ujao.