WEMA SEPETU KUTOKA KUITWA TASA HADI KUPATA MTOTO
Juni 12, 2026 ni siku ambayo huenda haitafutika katika kumbukumbu za msanii wa filamu Tanzania, Wema Sepetu. Baada ya miaka mingi ya machozi, maombi, matibabu na maneno ya kejeli kutoka kwa baadhi ya watu, hatimaye ndoto yake ya kuwa mama imetimia baada ya kujifungua mtoto wa kiume na mchumba wake, Whozu.
Habari za kujifungua kwa Wema zimepokelewa kwa furaha kubwa na mashabiki wake, lakini nyuma ya furaha hiyo kuna simulizi ndefu ya mwanamke aliyepitia majaribu mengi katika safari ya kutafuta mtoto.
Kwa miaka mingi, Wema amekuwa mmoja wa mastaa waliokuwa wakikabiliwa na maswali yasiyoisha kuhusu uzazi. Wakati wengine wakifurahia familia na watoto, yeye aliendelea kusubiri jambo ambalo aliliomba kwa muda mrefu.
Licha ya mafanikio yake katika tasnia ya filamu na biashara mbalimbali, Wema hakuwahi kuficha kuwa kuna kitu kilikuwa kinakosekana katika maisha yake.
Katika mahojiano mbalimbali aliyowahi kufanya kwa nyakati tofauti, Wema alikiri kuwa mama ilikuwa ndoto yake kubwa kuliko vitu vingi ambavyo tayari alikuwa amevipata maishani.
Mara kadhaa alizungumza kwa hisia kuhusu namna alivyokuwa akiomba na kusubiri siku ambayo angeitwa mama.
Kadri miaka ilivyokuwa ikisonga mbele, ndivyo presha kutoka kwa jamii ilivyozidi kuongezeka.
Kejeli za utasa na mgumba
Kutopata mtoto kwa muda mrefu kulimfanya Wema kuwa mmoja wa watu waliokuwa wakijadiliwa sana mitandaoni.
Baadhi ya watu walimwita tasa, wengine wakamwita mgumba huku wengine wakitumia suala hilo kama silaha ya kumdhalilisha.
Kejeli hizo zilikuwa zikimuumiza zaidi kwa sababu yeye mwenyewe alikuwa anatamani kupata mtoto kuliko hata waliokuwa wakimsema.
Katika ujumbe aliowahi kuandika mwaka 2023, Wema alikiri suala la watoto lilikuwa miongoni mwa mambo yaliyokuwa yakimuumiza zaidi moyoni.
Aliwahi kueleza wakati mwingine alikuwa anakwepa sehemu au matukio yanayohusisha watoto kwa sababu yalikuwa yanamkumbusha jambo ambalo moyo wake ulikuwa ukilitamani kwa muda mrefu.
Kauli hiyo iliwagusa mashabiki wengi waliogundua kuwa nyuma ya tabasamu la staa huyo kulikuwa na maumivu makubwa ambayo wengi hawakuyajua.
Tatizo la afya lililomweka kwenye wakati mgumu
Mwaka 2018, Wema alifunguka kuhusu changamoto ya kiafya iliyokuwa ikichangia safari yake kuwa ngumu zaidi.
Alieleza alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa mfumo wa uzazi uliohusishwa na matatizo katika ovari zake, hali iliyokuwa ikiathiri uwezo wake wa kushika mimba.
Kutokana na hali hiyo, alisafiri hadi India kwa ajili ya matibabu maalumu na alifanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye ovari zake.
Kwa mwanamke ambaye tayari alikuwa na kiu ya kupata mtoto, taarifa hizo zilimvunja moyo.
Wakati mashabiki walipokuwa wakimwona kwenye ‘red carpet’ na shughuli mbalimbali za burudani, ndani yake alikuwa akipambana na hofu ya kutotimiza ndoto yake ya kuwa mama.
Matumaini mapya baada ya matibabu
Baada ya kufanyiwa upasuaji na kuendelea na matibabu, Wema hakukata tamaa. Aliendelea kufuata ushauri wa madaktari huku akiweka matumaini yake kwa Mungu.
Mwaka 2019, alizungumza kwa furaha baada ya kueleza madaktari walikuwa wamempa matumaini mapya kuhusu uwezo wake wa kupata mtoto.
Kwa mara nyingine, moyo wake ulianza kuamini kuwa ndoto aliyokuwa akiisubiri kwa muda mrefu ingeweza kutimia. Hata hivyo, safari hiyo bado haikuwa imefika mwisho.
Mimba iliyoharibika
Wakati matumaini yakionekana kurejea, Wema alikutana na pigo jingine.
Katika maelezo yaliyowahi kutolewa na Whozu, ilielezwa Wema aliwahi kushika ujauzito lakini baadaye ukaharibika.
Tukio hilo lilikuwa pigo kubwa kwa wawili hao kwa sababu lilionekana kama hatua muhimu kuelekea ndoto yao ya kupata mtoto.
Kupoteza ujauzito kulimuumiza Wema ambaye tayari alikuwa amesubiri kwa muda mrefu kuona ndoto yake ikitimia. Lakini hata baada ya maumivu hayo, hakukubali kushindwa.
“Naitamani sana mimba”
Mwaka 2023, baada ya kusambaa kwa taarifa alikuwa mjamzito, Wema alikanusha uvumi huo.
Hata hivyo, katika maelezo yake aliweka wazi jambo moja.
Kwamba bado alikuwa akiitamani sana mimba.
Aliwaomba mashabiki wake waendelee kumuombea na kueleza kuwa bado alikuwa na matumaini ya kuwa mama siku moja.
Katika maelezo hayo, aliwahi pia kusema angependa kupata mtoto wa kiume.
Wengi walichukulia kauli hiyo kama ndoto ya kawaida ya mwanamke mwenye hamu ya kuwa mama.
Lakini miaka michache baadaye, maneno hayo yamekuwa kweli.
Whozu akawa sehemu ya historia
Katika kipindi chote cha uhusiano wao, Whozu amekuwa miongoni mwa watu waliokuwa karibu zaidi na Wema.
Licha ya changamoto walizowahi kupitia kama wapenzi, wawili hao wameendelea kuwa pamoja hadi kufikia hatua ya kupata mtoto wao wa kwanza.
Kuzaliwa kwa mtoto huyo wa kiume kumemfanya Whozu kuwa sehemu muhimu ya simulizi ya maisha ya Wema ambayo kwa miaka mingi ilionekana kama ndoto isiyoweza kutimia.
Ushindi baada ya miaka ya machozi
Leo hii, Wema habebi tena simulizi ya mwanamke aliyekuwa akisubiri mtoto. Anabeba simulizi ya mwanamke aliyepitia majaribu, alidhihakiwa, alilia, alifanyiwa upasuaji, alipoteza ujauzito na wakati mwingine kukata tamaa, lakini hakuwahi kuacha kuamini.
Kutoka kuitwa tasa hadi kuitwa mama.
Kwa Wema Sepetu, Juni 12, 2026 si tarehe ya kawaida. Ni siku iliyofunga ukurasa wa maumivu ya miaka mingi na kufungua ukurasa mpya wa maisha yake.
Na kwa wanawake wengi wanaopitia changamoto za uzazi, simulizi yake imebeba ujumbe mmoja mkubwa; kwamba safari inaweza kuwa ndefu, machozi yanaweza kuwa mengi, lakini matumaini hayapaswi kufa.
Kutoka Kanumba hadi Whozu
Katika ulimwengu wa burudani Tanzania, jina lake limekuwa likihusishwa mara kwa mara na simulizi za mapenzi zilizovuta hisia za mashabiki na kuzua mijadala isiyoisha. Kwa miaka mingi, maisha yake ya kimapenzi yamekuwa yakifuatiliwa karibu kama sehemu ya tasnia yenyewe, yakihusisha mastaa wakubwa na watu wenye ushawishi mkubwa kwenye jamii.
Safari yake inaanzia mwishoni mwa miaka ya 2000 alipokuwa karibu na marehemu Steven Kanumba, mmoja wa waigizaji wakubwa waliowahi kutamba Bongo Movie. Uhusiano wao ulionekana kuvutia macho ya wengi kutokana na umaarufu wa pande zote mbili, na licha ya baadaye kutamatika, uliacha alama kubwa kwenye historia ya burudani nchini.
Baadaye, kati ya mwaka 2012 na 2014, Wema alijikuta tena kwenye penzi lililotikisa tasnia ya muziki na filamu akiwa na msanii Diamond Platnumz. Uhusiano huo ulikuwa gumzo kubwa nchini, ukiwa miongoni mwa mahusiano yaliyokuwa yakifuatiliwa zaidi na vyombo vya habari na mashabiki wa burudani.
Mwaka 2013, kulitokea taarifa zilizodai Wema kufunga ndoa ya siri na mfanyabiashara Yussuph Jumbe. Hata hivyo, taarifa hizo zilijaa utata baada ya kuibuka madai ya kutokukubalika kwa upande wa familia na hatimaye ndoa hiyo kutodumu, jambo lililoongeza zaidi mjadala kuhusu maisha yake binafsi.
Mwaka 2015, jina lake liliendelea kuwa kwenye ‘headlines’ baada ya kuhusishwa na mwanamitindo wa Namibia Luis Munana, kabla ya baadaye kuonekana karibu na mchekeshaji na mshindi wa Big Brother Africa, Idris Sultan. Uhusiano huo nao uliibua gumzo kubwa mitandaoni na kwenye vyombo vya habari vya burudani.
Mwaka 2018, Wema alihusishwa tena na mfanyabiashara maarufu PCK na taarifa hizo ziliendelea kuonyesha jinsi maisha yake ya mapenzi yalivyokuwa yakivutia na kufuatiliwa kwa karibu na umma.
Katika miaka ya hivi karibuni, Wema akahusishwa na msanii wa Bongo Fleva, Whozu na kumekuwa na tetesi na mijadala mitandaoni kuhusu ukaribu wao na maisha ya mahusiano yao.
Baadhi ya mitandao ilikwenda mbali zaidi kwa kusambaza madai yasiyothibitishwa kuhusu ujauzito na hata taarifa za kujifungua, jambo lililozua taharuki na mjadala mkubwa, ingawa taarifa hizo zimekuwa zikichukuliwa kama sehemu ya tetesi za mitandaoni.
Licha ya kupitia mahusiano mbalimbali yaliyotikisa tasnia na kuzungumzwa sana, Wema ameendelea kubaki kuwa mmoja wa mastaa wanaovutia zaidi kwenye tasnia ya burudani, huku maisha yake ya mapenzi yakiendelea kuwa simulizi isiyo na mwisho mbele ya macho ya umma. Hongera kwa Wema na Whozu.