MASALANGA, KALAMBO WAWEKEZA NGUVU KUINUA VIPAJI
MAKIPA Hussein Masalanga wa Yanga na Aaron Kalambo wa Transit Camp FC wameamua kuweka nguvu zao katika kuendeleza makipa chipukizi kufikia ndoto zao.
Makipa hao wameamua kuanzisha kituo cha soka cha magolikipa mkoani Dodoma ambapo wanatarajia kufanya majaribio kuanzia Julai 17 hadi 24 watachukua wanaume na wanawake.
Masalanga alisema wataanza na magolikipa 30 ambao watakuwa na umri wa miaka 17 hadi 24 kati ya hao 10 watawachukua kuanzia miaka 17 hadi 24 na 20 miaka 8-17.
Alisema wana mipango mikubwa huko mbeleni, ila kwa sasa wachezaji watakuwa wanatoka nyumbani na kwenda mazoezini, wakipata wadhamini wa kutosha basi mambo yatabadilika.
“Nyumbani kwangu ni Dodoma, nikirudi likizo naona jinsi ambavyo vijana wengi wana vipaji vikubwa vinavyohitaji kushikwa mkono, hilo ndilo lililotupa msukumo mimi na Kalambo na sisi kuweka alama kwa wengine,” alisema na kuongeza;
“Kwa sasa kituo hicho tutakiita Kriniki ya Magolikipa, huko mbeleni tutajua tukiitaje, tayari tumemalizana na makocha wa kuwafundisha Michael Mfaume ‘Gege’ aliwahi kufundisha Fountain Gate Princess na Simba Queens na Ally Boniphace pia aliwahi kuifundisha timu ya FG ya wanawake na Alliance Girls, ukiachana na hao tunaendelea kufanya mazungumzo na makocha wenye CV kubwa ambao kwa sasa hawana timu”.
Naye Kalambo alisema:”Tunajifunza kuacha legasi kwa wengine, wakati tunaanza kucheza tulishikwa mkono na sisi lazima tuwainue waliyo chini yetu.”
Masalanga aliyejiunga na Yanga Januari 18, 2026 amewahi kucheza Singida Black Stars, TRA kipindi hicho ikiitwa Tabora United, Dodoma Jiji na Taifa Stars, huku Kalambo amezidakia Coastal Union,Geita Gold, Dodoma Jiji na Tanzania Prisons.
Wachezaji wengine waliyowahi kufanya hivyo ni nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto na kiungo Zawadi Mauya ambapo wana kituo chao kinachoitwa Mwamnyeto Foundation.