Pacome Afanyiwa Upasuaji, Wiki Sita Chini Ya Uangalizi
MSEMAJI wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, amesema kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Pacome Zouzoua, amefanyiwa upasuaji kwa mafanikio baada ya kupata jeraha kubwa, huku kwa sasa akiendelea vizuri chini ya uangalizi wa madaktari.
Kamwe amesema mara baada ya Pacome kuumia, jopo la madaktari wa Yanga kwa kushirikiana na madaktari wa Hospitali ya Aga Khan lilifanya uchunguzi wa kina kubaini ukubwa wa tatizo hilo, ambapo walikubaliana kuwa suluhisho sahihi lilikuwa ni kumfanyia upasuaji wa haraka.
Ameeleza kuwa upasuaji huo ulifanyika majira ya saa nane usiku na kukamilika kwa mafanikio, hatua inayompa Pacome nafasi ya kuanza rasmi safari ya kupona.
“Pacome alipata jeraha kubwa lililohitaji matibabu ya haraka. Baada ya tathmini iliyofanywa na madaktari wa klabu kwa kushirikiana na madaktari wa Hospitali ya Aga Khan, ilikubaliwa afanyiwe upasuaji,” ameseema Kamwe.
Kamwe amesema kiungo huyo sasa ataendelea kuwa chini ya uangalizi wa karibu wa madaktari kwa kipindi cha wiki sita, kabla ya kufanyiwa tathmini nyingine itakayobainisha hatua ya maendeleo yake na muda utakaohitajika ili kurejea uwanjani.
Amewahakikishia wanachama na mashabiki wa Yanga kuwa klabu itaendelea kutoa taarifa rasmi kuhusu maendeleo ya afya ya Pacome, huku akiwasihi waendelee kumuombea ili apone haraka na kurejea uwanjani akiwa na afya njema.