England Yahaha Kumzuia Erling Haaland
MIAMI, MAREKANI: BEKI wa England, Marc Guehi amesema anafurahia changamoto ya kumkabili mshambuliaji hatari wa Norway, Erling Haaland, lakini rekodi yake dhidi ya nyota huyo inaonyesha kazi inayomsubiri si rahisi hata kidogo.
Hata hivyo, maumivu hayo yamebakia historia katika ngazi ya klabu baada ya Guehi kujiunga na Manchester City akitokea Crystal Palace kwa ada ya pauni20 milioni mwezi Januari, hatua iliyowafanya wawili hao kuwa wachezaji wa timu moja.
Lakini urafiki huo hautakuwa na maana watakapokutana Jumamosi katika robo fainali ya Kombe la Dunia mjini Miami, ambapo Haaland anatarajiwa kuiongoza safu ya ushambuliaji ya Norway dhidi ya England.
Changamoto ya Guehi inaongezeka zaidi kutokana na kuwa tayari ana kadi moja ya njano. Akionyeshwa kadi nyingine dhidi ya Norway, atakosa mchezo wa nusu fainali iwapo England itafuzu.
Mbali na Guehi, wachezaji wengine wa England walio katika hatari ya kusimamishwa ni Declan Rice, Nico O’Reilly na Jude Bellingham, jambo linalompa wakati mgumu kocha Thomas Tuchel katika kupanga kikosi chake.
Kazi kubwa ya Tuchel ni kutafuta njia ya kufanya jambo ambalo hakuna timu iliyofanikiwa kufanya katika Kombe hili la Dunia, kumzuia Haaland kufunga.
Mshambuliaji huyo mwenye urefu wa futi 6 na inchi 5 amefunga katika kila mechi nne alizocheza kwenye mashindano haya, huku akipumzishwa katika mchezo wa mwisho wa makundi dhidi ya Ufaransa. Tayari ana mabao saba na ndiye mmoja wa vinara wa ufungaji.
Shangwe yake ya kupiga ngoma na kuongoza wachezaji pamoja na mashabiki wa Norway kusherehekea kwa mtindo wa makasia ya Waviking imekuwa moja ya alama za mashindano haya, baada ya kila ushindi wa timu yake.
Katika safu ya ulinzi ya England, Guehi anatarajiwa kuanza sambamba na Ezri Konsa katikati ya ulinzi, huku wawili hao wakipewa jukumu la kumdhibiti Haaland.
Tofauti na Guehi, Konsa ana rekodi nzuri zaidi dhidi ya mshambuliaji huyo.
Katika mechi tano ambazo Haaland amekutana na Konsa wakati Manchester City ikicheza dhidi ya Aston Villa, City imeshinda mara moja tu, huku Haaland akifunga bao moja pekee, ambalo lilikuja katika mechi yao ya kwanza mwezi Septemba 2022.
Zaidi ya hapo, Aston Villa imeshinda mechi tatu zilizopita dhidi ya Manchester City ambazo Konsa na Haaland walicheza pamoja.
Kwa upande wa Guehi, kumbukumbu mbaya zaidi ni mwaka 2022 pale Haaland alipofunga mabao matatu (hat-trick) dhidi ya Crystal Palace, akionyesha ubora wake mbele ya beki huyo.
Hata hivyo, Guehi pia ana sababu ya kujivunia kwani ameshinda mara tatu dhidi ya Haaland, idadi inayolingana na ushindi wa mshambuliaji huyo katika mikutano yao.
Ushindi maarufu zaidi ulikuwa katika fainali ya Kombe la FA mwaka 2025, ambapo Crystal Palace iliifunga Manchester City bao 1-0 na kutwaa taji lake la kwanza kubwa katika historia ya klabu hiyo.
Beki mwingine anayemfahamu vizuri Haaland ni John Stones, ambaye walicheza pamoja Manchester City kwa miaka minne.
Kutokana na kuumia kwa Jordan Henderson kwenye kifundo cha mkono, Tuchel anafikiria kumtumia Stones kama mbadala wa Elliot Anderson katika safu ya kiungo.
Iwapo atapewa nafasi hiyo, Stones atakuwa na kumbukumbu nzuri dhidi ya Haaland. Mwaka 2021, wakati Haaland akiwa Borussia Dortmund, alishindwa kufunga katika mechi zote mbili za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Manchester City ya Stones.
Licha ya kusumbuliwa na majeraha mara kwa mara katika miaka ya hivi karibuni, Stones amesema yuko fiti na tayari kwa pambano hilo.
Baada ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Mexico, hata aliwachekesha wenzake kwa kujifanya ameumia bega kabla ya kuanza kucheza na kuimba katika vyumba vya kubadilishia nguo.
Beki mrefu, Dan Burn pia anaweza kuwa chaguo la baadaye kutokana na urefu wake wa futi 6 na inchi 7, ingawa nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza inaonekana kuwa ndogo.
Rekodi yake dhidi ya Haaland pia si mbaya. Ingawa Newcastle haijawahi kuifunga Manchester City katika mechi nane ambazo Burn na Haaland walicheza pamoja, mshambuliaji huyo amefunga bao moja pekee dhidi yake.
England inaingia katika mchezo huu ikiwa na morali kubwa baada ya kuiondoa Mexico kwa ushindi wa mabao 3-2 licha ya kucheza na wachezaji 10 kwa sehemu ya mchezo.
Akizungumzia ushindi huo, Guehi amesema nguvu kubwa ya timu hiyo ni umoja.
“Tunazungumza kuhusu mshikamano wa timu hii, na kila mmoja aliuonyesha katika mchezo ule. Si wale walioanza pekee, bali kila aliyepata nafasi na hata wale ambao hawakuingia uwanjani walitupa sapoti kubwa. Ulikuwa ushindi wa timu nzima,” amesema.
Sasa Tuchel anahitaji mshikamano huo kujirudia tena ikiwa England inataka kumzuia Haaland katika joto kali la Miami na kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia.